Pata taarifa kuu

Japani: Polisi yachunguza uwezekano wa uzembe baada ya ndege mbili kugongana

Polisi wa Japan wanachunguza kubaini iwapo ajali ya ndege mbili kugongana kati ya ndege ya shirika la ndege la Japan Airlines na ndege ndogo ya walinzi wa pwani ya Japan ambayo ilisababisha vifo vya watu watano siku ya Jumanne Januari 2 mjini Tokyo ulitokana na uzembe, vyombo vya habari kadhaa vimeripoti leo Jumatano.

Japani, uwanja wa ndege wa Tokyo-Haneda Januari 2, 2024: picha ya ndege ya shirika la ndege la Japan Airbus ikiwaka moto baada ya kugongana na dege ya walizi wa pwani ya Japan kwenye uwanja wa ndege wa Tokyo-Haneda tarehe 1 Januari.
Japani, uwanja wa ndege wa Tokyo-Haneda Januari 2, 2024: picha ya ndege ya shirika la ndege la Japan Airbus ikiwaka moto baada ya kugongana na dege ya walizi wa pwani ya Japan kwenye uwanja wa ndege wa Tokyo-Haneda tarehe 1 Januari. REUTERS - ISSEI KATO
Matangazo ya kibiashara

Abiria 379 na wafanyakazi wa ndege ya shirika la ndege la Japan Airlines iliyoshika moto Jumanne kwenye uwanja wa ndege wa Tokyo-Haneda waliondolewa salama, baada ya kugongana kwenye lami ya uwanja huo wa ndege na ndege ndogo ya walinzi wa pwani ya Japan, watano kati ya sita waliokuwa ndani yake walifariki dunia. Rubani alifanikiwa kujiokoa, ingawa alijeruhiwa vibaya.

Agizo kinzani zilizotolewa na maafisa wa suala la usafiri wa anga?

Ajali hii ilitokea wiki chache tu baada ya tasnia ya Usafiri wa anga duniani kupokea maonyo mapya kuhusu usalama wa njia za kutua na kurukia ndege.

Ndege hii ndogo ya walinzi wa pwani ya Japan ilikuwa ikijiandaa kuondoka ili kutoa bidhaa muhimu kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi la Jumatatu katika idara ya Ishikawa (katikati ya Japani), ambalo lilisababisha vifo vya takriban watu 62 kulingana na ripoti mpya ya muda iliyotolewa leo Jumatano asubuhi.

Japan Airlines ilisema katika taarifa siku ya Jumanne kwamba Airbus ilipokea mara kadhaa kibali cha kutua kabla ya kukaribia. Rekodi za udhibiti wa usafiri wa anga zinazopatikana kwenye tovuti ya LiveATC.net na ambazo shirika la habari la AFP liliweza kuona nazo zinaonyesha kuwa ndege ya Japan Airlines iliidhinishwa kutua saa 11:45 jioni saa za Japan, dakika chache kabla ya ajali hiyo kutokea, kulingana na mamlaka.

"Japan 516, endelea na kusogelea kituo cha kuegesha," alisema afisaa mmoja masuala ya usafiri wa anga siku ya Jumanne saa 11:43 jioni saa za ndani, dakika nne kabla ya ajali hiyo kutokea.

Kinyume chake, Wakati huo huo mamlaka ya masuala ya usafiri wa anga iliomba ndege ya walinzi wa pwani kusubiri mbali na njia za kutua na kurukia ndege, kulingana na kituo cha televisheni cha taifa cha NHK, kikinukuu chanzo ndani ya Wizara ya Usafiri ya Japani. Lakini kulingana na afisa wa walinzi wa pwani pia aliyenukuliwa na NHK, kamanda wa ndege hiyo alibaini baada ya ajali hiyo kuwa alipata kibali cha kuruka.

Sababu halisi hazijulikani kufikia sasa

Mamlaka ya Japani imesema sababu za ajali hiyo bado hazijajulikana. Chunguzi mbili tofauti zinaendelea, mmoja ukiendeshwa na polisi ya Japani, mwingine na ukifanywa na Bodi ya Usalama wa Usafiri nchini Japani (JTSB). Shirika la ndege la Japan Airlines, Walinzi wa Pwani na Wizara ya Uchukuzi ya Japan kwa sasa wanakataa kutoa maoni zaidi kuhusu tukio hili, kwa sababu ya uchunguzi unaoendelea.

Kulingana na shirika la habari la Japan la Kyodo, vinasa sauti vya ndege ya walinzi wa pwani tayari vimepatikana na JTSB. Timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Upelelezi na Uchambuzi wa Usafiri wa Anga kutoka Ufaransa (BEA) inatarajiwa kuwasili Japan siku ya Jumatano kushiriki uchunguzi wa ajali hiyo, ikizingatiwa kuwa ndege ya JAL ilikuwa Airbus A350 -900, iliyotengenezwa Toulouse (kusini-magharibi mwa Ufaransa).

Airbus pia ilitangaza kwamba itatuma timu ya wataalamu kutoa "msaada wa kiufundi" kwa Bodi ya Usalama ya Usafiri wa Japani (JTSB), inayohusika na uchunguzi.

Usafiri wa anga bado umetatizwa

Usafiri kwenye uwanja wa ndege umeendelea kuzorota Jumatano asubuhi, hasa kwa ndege zinazofanya safari za ndani, ambazo karibu safari 70 zimefutwa katika sehemu ya kwanza ya siku, kulingana na tovuti yake.

Japan Airlines pia imetangaza kwenye ukurasa wake wa X (zamani ikiitwa Twitter) kwamba "kwa kuzingatia athari za ajali hii, tikiti za ndege za wateja walioweka nafasi ya safari za ndege za shirika la ndege la JAL kabla ya Machi 31 zinaweza kurejeshwa bila malipo" .

Ajali zinazohusisha ndege za abiria ni nadra sana nchini Japani. Mbaya zaidi kati ya ajali hizi ilitokea mnamo mwaka 1985, wakati ndege ya Japan Airlines ilipoanguka kati ya Tokyo na Osaka, na kuua watu 520.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.