Pata taarifa kuu

Ukraine: Mashambulio mapya ya Urusi yaacha kaya milioni 1 bila umeme

Zaidi ya kaya milioni moja hazina umeme nchini Ukraine kufuatia mashambulizi mapya ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati nchini humo, mamlaka ya Ukraine imetangaza Jumamosi Oktoba 22.

Wateja katika duka kuu la Kyiv, ambalo halina umeme baada ya shambulio jipya la Urusi, Oktoba 22, 2022.
Wateja katika duka kuu la Kyiv, ambalo halina umeme baada ya shambulio jipya la Urusi, Oktoba 22, 2022. REUTERS - GLEB GARANICH
Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi mapya ya Urusi yamelenga miundombinu ya nishati magharibi mwa Ukraine siku ya Jumamosi, huku maafisa wa Ukraine wakiripoti kukatwa kwa umeme katika maeneo kadhaa ya nchi. Vikosi vya Urusi "vilifanya shambulio jipya kwa makombora kwenye mitambo ya nishati ya maeneo makuu katika mikoa ya magharibi mwa Ukraine", shirika la umeme nchini Ukrainela Ukrenergo limebaini kwenye mitandao ya kijamii, kabla ya kuongeza kuwa ukubwa wa uharibifu huo "unalinganishwa" au unaweza "kuzidi athari ya shambulio la Oktoba 10 na 12".

Vikwazo vya nishati "vinatumika kwa nguvu" katika mikoa kadhaa, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa kyiv na jimbo lake, shirika la umeme la Ukrenergo limesema, likiahidi kwamba wataalamu wake "wanachukua hatua zote kurejesha umeme haraka iwezekanavyo katika mikoa ambayo sasa haina umeme".

Wakati huo huo, Waukraine tayari wamepunguza kwa hiari matumizi yao ya umeme kwa 5% hadi 20% kwa wastani kwa baadhi ya siku na katika baadhi ya maeneo, mkuu wa Ukrenergo Volodymyr Kudrytsky ameliambia shirika la habari la AFP katika taarifa iliyoandikwa.

Maafisa kote nchini walikuwa wameripoti awali kukatwa kwa umeme baada yashambulizi jipya. Upande wa magharibi, umeme na maji vilikatika katika baadhi ya maeneo ya eneo la Volyn, kulingana na gavana wa mkoa huo. Mji wa Khmelnytsky haua umeme na maafisa wa jiji walitoa wito kwa wakaazi kujiandaa kwa kukatwa kwa maji.

Katika eneo la Rivne, pia upande wa magharibi, Gavana Vitali Koval amesema mashambulizi yamelenga "miundombinu ya nishati" ya mkoa huo asubuhi, na kuharibu vituo vya umeme. Kukatika kwa umeme pia kumeripotiwa katika eneo la Odessa (Kusini-Magharibi) baada ya "mashambulio mawili ya makombora kwenye miundombinu ya nishati ya mkoa huo", amesema Gavana Maxim Marchenko.

Gavana wa mkoa wa Kirovohrad, katikati mwa nchi, kwa upande wake amewataka wafanyabiashara na wakaazi wa mkoa huo kupunguza matumizi yao ya umeme baada ya shambulio dhidi ya miundombinu "muhimu" ya nishati.

Tangu Oktoba 10, Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi ikilenga miundombinu na mitambo ya umeme na maji nchini Ukraine.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.