Pata taarifa kuu
USALAMA-MAUAJI

Mashambulizi dhidi ya kambi ya watu waliokimbia makazi yao Nigeria, wahanga walikatwa vichwa

Mamlaka ya Nigeria siku ya Ijumaa imeripoti shambulio katika jimbo la Benue ambalo lilisababisha vifo vya takriban watu wanane; baadhi ya wahanga walikatwa vichwa. 

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abagena katika jimbo la Benue nchini Nigeria mnamo Aprili 11, 2018.
Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abagena katika jimbo la Benue nchini Nigeria mnamo Aprili 11, 2018. REUTERS/Afolabi Sotunde/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Mshauri wa Usalama wa Jimbo la Benue nchini Nigeria Paul Hemba amezungumza kwenye kituo cha televisheni cha Channels TV chenye makao yake mjini Lagos siku ya Ijumaa ambapo amesema shambulio lilifanyika mkabala na kambi ya Abagana kwa ajili ya watu waliokimbia makazi yao, katika mji wa Markudi, siku ya Alhamisi jioni.

Kulingana na Paul Hemba, watu waliokuwa na silaha waliwaua watu 8 na kuwajeruhi wengine 8. Baadhi ya wahanga walikatwa vichwa, amesema.

Kulingana na  VOA ikinukuu mamlaka za eneo hilo, hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini wanashuku kuwa lilitekelezwa na wafugaji wa kabila la Fulani.

Mamlaka pia zinasema kuwa Jimbo la Benue na Jimbo jirani la Nassarawa yameshuhudia makabiliano kadhaa kati ya wakulima na wafugaji, makabiliano ambayo yamesababisha hasara nyingi.

Shambulio la Alhamisi ni shambulio la pili kutekelezwa karibu na kambi ya Abagana katika kipindi cha miaka miwili, la kwanza lilifanyika mwaka 2021 na kusababisha vifo vya watu saba.

Msemaji wa polisi wa jimbo la Benue Yar Sewuese amesema mamlaka inachunguza shambulio la hivi.

"Kwa wakati huu, ninaweza tu kuthibitisha kwamba kulikuwa na shambulio jana usiku na polisi wako kwenye eneo la tukio," Yar Sewuese amesema.

"Watu wengine waliuawa, wengine walijeruhiwa, na kamishna yuko njiani," ameongeza msemaji wa polisi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.