Pata taarifa kuu

Rais Déby ateua wabunge 104 zaidi katika bunge la Chad

Jenerali Mahamat Idriss Déby Itno, ambaye hivi majuzi aliteuliwa tena kwa miaka miwili kama rais wa Chad baada ya kuchukua mamlaka kufuatia kifo cha babake mwaka 2021, ameteua Jumatatu kwa agizo la kirais wabunge 104 zaidi wa bunge la mpito.

Mahamat Idriss Deby Itno anahudhuria hafla ya kuhitimisha kongamano Jumuishi la mazungumzo ya kitaifa (DNIS), mjini N'Djamena mnamo Oktoba 8, 2022.
Mahamat Idriss Deby Itno anahudhuria hafla ya kuhitimisha kongamano Jumuishi la mazungumzo ya kitaifa (DNIS), mjini N'Djamena mnamo Oktoba 8, 2022. AFP - DENIS SASSOU GUEIPEUR
Matangazo ya kibiashara

Mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa (DNIS), ambayo yalimpa miezi 24 zaidi kama rais wa mpito, yalipendekeza kuongeza idadi ya wabunge kutoka 93 hadi 197 katika Baraza la Kitaifa la Mpito (CNT), ambalo ni kama Bunge la mpito tangu Bw. Déby kutangazwa kuwa mkuu wa nchi kwa mara ya kwanza tarehe 20 Aprili 2021, akiwa akiongoza majenerali 15.

Upanuzi wa CNT unalenga kuwaunganisha watu binafsi kutoka vyama, mashirika ya kiraia na vuguvugu la waasi ambao walikuwa wamejitokeza kwenye mazungumzo haya ya kitaifa yaliyosusiwa na sehemu kubwa ya upinzani na miongoni mwa makundi yenye silaha yenye nguvu zaidi. Makundi haya yanalaani kile yanachokiita "muendelezo wa utawala wa kifalme" nchini Chad, ulioongozwa kwa miaka 30 kwa mkono wa chuma na Idriss Déby Itno, babake Mahamat, aliyeuawa katika uwanja wa mapigano dhidi ya waasi mwaka mmoja na nusu uliopita.

Katika agizo hilo la kirais ambalo shirika la habari la AFP lilipata kopi, Jenerali Déby aliteua "wajumbe 104 wapya wa CNT" siku ya Jumatatu, wakiwemo wawakilishi wa upinzani wa zamani ambao waliungana na serikali wakati wa mazungumzo ya kitaifa na makundi ya waasi yaliyotia saini makubaliano ya amani mwezi Agosti.

Mnamo Aprili 20, 2021, kundi la majenerali 15 lilitangaza kifo cha Marshal Idriss Déby na kumtangaza mtoto wake Mahamat, jenerali wa umri wa miaka 37 wakati huo, "Rais wa Jamhuri" kwa kipindi cha "mpito" cha miezi 18, ambacho kinaweza kuongezwa mara moja hadi utakapo fanyika "uchaguzi huru na wa kidemokrasia".

Majenerali waliifuta Katiba, wakaifuta serikali na kuvunja bunge, na kuunda CNT yenye wajumbe 93, kuchukua nafasi yake miezi mitano baadaye, wajumbe ambao waliteuliwa na mkuu mpya wa N'Djamena. "Bunge" hili la mpito linawajibika hasa kuandaa katiba mpya na kuandaa uchaguzi.

Mahamat Déby alipokea uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa - Ufaransa, Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU)- ambao hata hivyo ulidai kwamba kipindi cha mpito kisichozidi miezi 18, pia kuhakikisha kwamba Jenerali Déby amejitolea kutowania katika chaguzi zijazo.

Miezi kumi na minane baadaye, DNIS sio tu ilimuongeza tena kipindi kingine cha kutawala kwa miaka miwili akiwa rais wa Chad lakini pia ilimuidhinisha kuwa kiongozi mkuu na amiri jeshi mkuu kwa kipndi cha miaka miwili.

Tarehe 20 Oktoba mwaka huu, maandamano ya upinzani yaliyokandamizwa kwa nguvu yalisababisha vifo vya takriban watu hamsini katika miji mikuwa ya nchi, zaidi ya 300 kujeruhiwa na mamia ya watu walikamatwa. EU "ililaani vikali" "matumizi ya nguvu kupita kiasi" na "mashambulio makubwa dhidi ya uhuru wa kujieleza".

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.