Pata taarifa kuu
MAZUNGUMZO-AMANI

Ethiopia / Tigray: Pande hasimu zakubaliana 'kusitisha mapigano'

Serikali ya Ethiopia na waasi katika eneo la Tigray wamekubaliana "kusitishwa mapigano" katika eneo hili la kaskazini mwa Ethiopia, ambalo limekumbwa na mzozo kwa miaka miwili, wakati wa mazungumzo mjini Pretoria, Umoja wa Afrika (AU) umesema siku ya Jumatano. 

Mwakilishi wa serikali ya Ethiopia Redwan Hussein Rameto (kushoto) na mwakilishi wa Tigray Getachew Reda wakipeana mikono baada ya kusainiwa kwa mkataba wa amani mjini Pretoria mnamo Novemba 2, 2022.
Mwakilishi wa serikali ya Ethiopia Redwan Hussein Rameto (kushoto) na mwakilishi wa Tigray Getachew Reda wakipeana mikono baada ya kusainiwa kwa mkataba wa amani mjini Pretoria mnamo Novemba 2, 2022. AFP - PHILL MAGAKOE
Matangazo ya kibiashara

"Pande zote mbili katika mzozo wa Ethiopia zimekubali rasmi kusitisha mapigano,"  amesema Olusegun Obasanjo, Mwakilishi Mkuu wa AU katika Pembe ya Afrika, katika mkutano na waandishi wa habari.

Makubaliano haya yanaashiria "mwanzo wa enzi mpya kwa Ethiopia", ameongeza.

Wajumbe kutoka serikali ya shirikisho ya Ethiopia na waasi walikuwa wakikutana chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika (AU) tangu Oktoba 25 huko Pretoria, nchini Afrika Kusini. Mkutano huu ni wa kwanza kufanywa hadharani kati ya kambi hizo mbili.

Waasi pia wamekaribisha mpango huo. "Ili kukabiliana na mateso ya raia wetu, tumefanya makubaliano, kwa sababu tunapaswa kujenga uaminifu," kiongozi wa ujumbe wa waasi Getachew Reda amesema.

Akithibitisha nia yake ya "kutekeleza makubaliano haraka iwezekanavyo", amesisitiza "nia ya pande hizo mbili kusahau yaliyopita ili kuanda njia mpya kuelekea amani".

Waasi wa Tigray na jeshi la shirikisho - wakisaidiwa na vikosi kutoka mikoa jirani na jeshi la Eritrea, nchi inayopakana na jimbo la Tigray - wamekuwa wakipigana tangu mwezi Novemba 2020.

Baada ya mapatano ya miezi mitano, mapigano yalianza tena mwezi Agosti. Vikosi vya Ethiopia na Eritrea vilitangaza hivi karibuni kuwa vimeteka miji kadhaa ya jimbo la Tigray. Mzozo huo umechangiwa na dhuluma dhidi ya raia, kulingana na shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International.

Kuanza tena kwa mapigano, ambayo yanatatiza utoaji wa misaada ya kibinadamu, ambayo eneo hilo lenye wakazi milioni sita linahitaji, kumeitia wasiwasi jumuiya ya kimataifa. Mzozo huu mbaya umeingiza eneo hilo katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Hadi watu nusu milioni wameuawa, Umoja wa Mataifa unabaini. Zaidi ya Waethiopia milioni mbili wameyakimbia makazi yao na mamia ya maelfu ya watu kukumbwa njaa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.