Pata taarifa kuu
NIGERIA-USALAMA

Nigeria: Maafisa 19 wa vikosi vya usalama na ulinzi wauawa

Watu wenye silaha wamewauwa wanajeshi 13, maafisa watano wa polisi na mwanamgambo mmoja wa eneo hilo wakati wa mapigano makali kaskazini-magharibi mwa Nigeria, ambapo magenge ya "majambazi" yamekuwa yakiwatishia watu kwa miezi mingi,  kulingana na vyanzo vyausalama.

Vikosi vya ulinzi vya Nigeria katika jimbo la Zamfara.
Vikosi vya ulinzi vya Nigeria katika jimbo la Zamfara. © REUTERS/Afolabi Sotunde/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hilo lilitokea siku ya Jumanne katika kijiji cha Kanya, katika jimbo la Kebbi linalopakana na Niger. Siku ya Jumatatu, takriban watu 57 kutoka kundi la wanamgambo wa kujilinda waliuawa umbali wa kilomita chache, karibu na kijiji cha Sakaba, wilayani Zuru.

Kulingana na mashahidi, mamia ya "majambazi" walivamia kijiji cha Kanya Jumanne jioni katika eneo la Danko-Wasagu na kupigana kwa zaidi ya saa tatu na kikosi cha polisi na askari. "Walifika kwa pikipiki zipatazo 200, watu watatu wakitumia pikipiki moja," Musa Arkiza, ambaye ni mkazi wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP.

"Kulikuwa na maiti 19 - askari 13, maafisa watano wa polisi na mwanamgambo mmoja," mjumbe wa idara ya usalama ameliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina, akiongeza kuwa watu wengine wanane, wakiwemo wanajeshi wanne, walijeruhiwa na kupelekwa hospitali. "Mpigano yalidumu zaidi ya saa tatu, magaidi walikuwa na nguvu kubwa kutokana na idadi yao," ameongeza.

Majambazi watumia pikipiki

"Tunafikiri ni majambazi sawa na wale walioua wanamgambo" Jumatatu huko Sakaba, alisema Musa Arkiza. "Walivuka mto na kuizingira Kanya, na kushambulia maafisa wa usalama kutoka pande tatu," aliongeza.

Kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria kwa miaka kadhaa ni eneo la magenge mengi ya "majambazi" ambao hupora vijiji, kuwateka nyara watu ili kuwakomboa kwa fidia na kusababisha ugaidi miongoni mwa watu. Lakini hivi majuzi mashambulizi yameongezeka licha ya jeshi kujaribu kuwaondoa "majambazi" kutoka kambi zao.

Rais Muhammadu Buhari mwezi Januari alitoa wito wa kushughulikiwa kwa nguvu zaidi kijeshi dhidi ya magenge, ambayo sasa yametajwa kama "magaidi" na serikali. Jenerali huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 79 anakosolewa vikali kwa kutoweza kuzuia kuenea kwa ukosefu wa usalama nchini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.