Pata taarifa kuu

Nigeria yawahamisha raia wake kutoka nchi zinazopakana na Ukraine

Serikali ya Nigeria siku ya Jumatano imepanga kuanza kuwasafirisha kwa ndege zaidi ya raia wake 1,000 kutoka nchi jirani na Ukraine, ambako vita vimewalazimu kukimbia.

Watu wanaokimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine wakiwasili kwenye kituo cha treni huko Lviv, Ukrainia Machi 1, 2022.
Watu wanaokimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine wakiwasili kwenye kituo cha treni huko Lviv, Ukrainia Machi 1, 2022. REUTERS - THOMAS PETER
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Afrika ulilaani ripoti kwamba Waafrika wametendewa vibaya na katika baadhi ya kesi walinyimwa haki ya kuvuka mipaka ya Ukraine kwa ajili ya usalama, ukisema kuwa unyanyasaji kama huo ni "ubaguzi wa kutisha".

Ndege tatu zilizokodishwa na mashirika ya ndege ya nchini humo Max Air na Airpeace zitaondoka siku ya Jumatano, zikiwa na uwezo wa kuwarudisha karibu watu 1,300, wizara ya mambo ya nje ya Nigeria ilisema katika taarifa yake.

"Kundi la kwanza la raia hao wanatarajiwa kuwasili Nigeria Alhamisi, Machi 3," Gabriel Aduda, katibu mkuu wa wizara hiyo, amesema katika taarifa hiyo.

"Tunawahakikishia Wanigeria kwamba tunafanya kazi saa nzima ili kuhakikisha raia wetu wanarudishwa nyumbani salama," amesema.

Balozi wa Ukraine nchini Afrika Kusini alisema wiki hii kuwa nchi hiyo ina wanafunzi 16,000 kutoka Afrika, lakini wengi wao wanatoka nchi zisizo na balozi nchini Ukraine, jambo linalofanya hali kuwa ngumu.

Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ina wanafunzi 5,600 nchini Ukraine, kulingana na wizara hiyo.

Siku ya Jumanne, Ghana ilirudisha kundi lake la kwanza la wanafunzi 17 kati ya zaidi ya 500 kutoka nchi jirani za Ukraine.

Serikali mbalimbali, kuanzia Afrika Kusini hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinajaribu kuwasaidia raia wao, huku baadhi yao wakituma wanadiplomasia katika mipaka ya Ukraine kuwasaidia wanafunzi wanaolalamikia kukwama nchini Ukraine.

Milioni moja wakimbizi wa ndani

Kundi la wanafunzi wapatao 30 wa Cameroon ambao walikuwa hadi hivi majuzi katika mji wa kati wa Kirovograd nchini Ukraine wanasema ni katika siku za hivi majuzi tu ambapo walikabiliwa na ubaguzi wa rangi nchini Ukraine.

Kabla ya vita, waliiambia shirika la habari la AFP, kila kitu kilikuwa sawa, lakini baada ya uvamizi waliwekwa mbali na treni zinazoondoka nchini.

Maafisa wa Poland wanasema kila mtu alitendewa kwa usawa wakati wa kuvuka mpaka. Mamlaka ya uhamiaji nchini Ukraine pia ililiambia shirika la habari la AFP kwamba hakuna mtu aliyezuiwa kuondoka nchini humo.

Mbali na wakimbizi karibu 680,000 ambao tayari wameondoka Ukraine kuelekea mataifa jirani, inakadiriwa watu milioni moja wamekimbia makazi yao lakini bado wako ndani ya nchi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.