Umoja wa Mataifa wajaribu kusuluhisha pande zinazokinzana Sudan
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes amezindua mazungumzo yanayolenga kumaliza mvutano wa kisiasa nchini humo baada ya jeshi kuchukua madaraka na Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kujiuzulu.
Imechapishwa:
Mazungumzo hayo yanalenga kuwasaidia raia wa Sudan kujadiliana kuhusu kurejea kwenye njia ya demokrasia ili kumaliza mzozo unaoendelea.
Vuguvugu la Makundi mbalimbali ya kiraia yanayoshiriki kwenye maandamano yanayoendelea kushinikiza jeshi kuondoka madarakani, linasema halikufahamishwa kuhusu mpango huo wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, msemaji wa vuguvugu hilo Jaafar Hassan, amesema wapo tayari kushiriki kwenye mazungumzo hayo, iwapo yatalenga kuuundoa uongozi wa kijeshi na kurejeshwa kwa ule wa kiraia.
Muungano wa wasomi nao umekataa mpango huu wa Umoja wa Mataifa, ambao hata hivyo, umekaribishwa na mataifa ya Marekani, Uingereza, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Misri.
Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, litakutana kujadili hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan.