Pata taarifa kuu
SUDAN-USALAMA

Sudan: Mamia ya tani za chakula zaporwa katika ghala la Umoja wa Mataifa Darfur

Kielelezo kipya cha kuongezeka kwa ghasia zinazoikumba Darfur nchini Sudan: kundi lenye silaha lilishambulia, jioni ya Jumanne, Desemba 28, ghala la shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP. Hii ilitokea El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini. Mamia ya tani za bidhaa za chakula ziliporwa.

Nembo ya shirika la Umoja wa Mataifa Mpango wa Chakula Duniani.
Nembo ya shirika la Umoja wa Mataifa Mpango wa Chakula Duniani. AP - Robert Bumstead
Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa mji wa El Fasher walisikia milio ya risasi kwa mara ya kwanza jioni ya Jumanne, Desemba 28. Katika hali hiyo, mamlaka za mitaa ziliweka sheria ya kutotoka nje katika jiji hilo. Na ilikuwa ni Jumatano asubuhi tu ambapo Umoja wa Mataifa (UN) uliona uharibifu huo.

Shambulio hilo lililenga ghala la shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani ambalo lilikuwa na tani 1,900 za chakula, zilizokusudiwa kutolewa kwa wakazi walio hatarini zaidi wa Darfur. Ukaguzi unaendelea ili kubaini ukubwa wa kisa hicho cha uporaji. Na shambulio hili halijatengwa. Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani visa vya uporaji na ghasia karibu na kituo cha zamani cha Umoja wa Mataifa, katika mji wa El Fasher; kituo ambacho kilikuwa kimekabidhiwa kwa mamlaka nchini Sudan kama sehemu ya mpango wa kuondoka kwa UNAMID (Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur).

Msururu huu wa mashambulizi unatatiza shughuli za kibinadamu, hata kama mahitaji yameongezeka kwa kasi huko Darfur katika mwaka uliopita. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu waliokimbia makazi yao huko wameongezeka mara nane ikilinganishwa na mwaka jana. Makubaliano ya Juba, yaliyoafikiwa mwezi Oktoba 2020, yaliibua matumaini kwamba hatimaye Darfur itakuwa na amani. Na kwa sasa inaonekana kuwa hiyo ni ndoto.

Tangu mwezi Januari, mapigano ya umwagaji damu yameongezeka huko, huku kukiwa na hali ya kutokuadhibu, huku macho ya kimataifa yakilenga mji mkuu Khartoum na mzozo wa kisiasa uliochochewa na mapinduzi ya Oktoba 25.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.