Mazungumzo ya siasa kuhusu Uchaguzi wa Somalia yaanza
Viongozi wa siasa nchini Somalia wameanza mazungumzo ya kupata mwafaka wa namna ya kuandaa uchaguzi uliocheleweshwa nchini humo.
Imechapishwa:
Mbali na wanasiasa nchini humo, mazungumzo haya yanawashirikishia pia wawakilishi kutoka Jumuiya ya Kimataifa.
Uchaguzi nchini Somalia ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi Februari, lakini ikashindikana baada ya wanasiasa kushindwa kuelewana ni mfumo upi utumiwe kufanikisha uchaguzi huo.
Hali hiyo ilizua sintofahamu ya kisiasa nchini humo na kupelekea wabunge kumwongezea rais Mohamed Abdullahi Mohamed, anayefahamika pia kwa jina la Farmajo, kuongoza kwa miaka miwili zaidi, hatua iliyoshutumiwa na wapinzani na jumuiya ya Kimataifa.
I am chairing the National Electoral Consultative Summit that has commenced today. I thank the Presidents of the FMS & the Governor of Banadir for their participation. I am confident that it will conclude in a manner that steers our Great Nation towards triumphant trajectory. pic.twitter.com/nPKOjjAlB1
— Mohamed Hussein Roble (@MohamedHRoble) May 22, 2021
Mazungumzo yaliyoanza siku ya Jumamosi, yanaongozwa na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble huku washirika wakuu wakiwa ni viongozi wa majimbo matano nchini humo.
Usalama umeimarishwa mjini Mogadishu, wanajeshi wa Umoja wa Afrika AMISOM wameonekana wakipiga doria, kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanaendelea kwa usalama.
Haijafahamika ni lini mazungumzo haya yatamalizika na iwapo mwafaka utapatikana.