Pata taarifa kuu
ICC

Karim Khan ateuliwa kuwa mwendesha mashtaka ajaye wa ICC

Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) hatimaye zimemteuwa wakili wa Uingereza mwenye umri wa miaka 50, Karim Khan, kuwa mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo, baada ya Marekani kuchukuwa vikwazo dhidi ya mwendesha wa sasa Fatou Bensouda.

Mwendesha mashtaka wa ICC anayemaliza muda wake, Fatou Bensouda.
Mwendesha mashtaka wa ICC anayemaliza muda wake, Fatou Bensouda. Bas Czerwinski/Pool via REUTERS/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Karim Khan alichaguliwa dhidi ya wagombea wengine watatu kutoka Ulaya katika duru ya pili ya uchaguzi huo, akishinda kwa kura 72 kwa jumla ya kura 122 zilizopigwa.

Karim Khan ambaye ni mtaalam wa haki za binadamu, hivi karibuni aliongoza uchunguzi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu wa kundi la Islamic State. Wakati wa uchunguzi huo, alibaini kwamba vitendo vya kundi hilo vinafanana na vile vya viongozi wa Kinazi huko Nuremberg.

Tarehe 16 Juni, atamrithi Mwanasheria Mkuu anayemaliza muda wake, Fatou Bensouda, kutoka Gambia, ambaye alifanya uchunguzi wa kutatanisha, hasa kuhusu mzozo wa Israeli na Palestina na nchini Afghanistan.

Karim Khan amewahi kuwa wakili wa upande wa utetezi katika kesi nyingi za ICC, ikiwa ni pamoja na kesi ya mtoto wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, Seif al-Islam. Kwanza alifundishwa sheria ya kimataifa katika Mahakama ya zamani ya Uhalifu wa kivita kwa Yugoslavia ya zamani, ambapo aliwahi kuwa mshauri wa sheria kwa ofisi ya mwendesha mashtaka. Halafu alisimamia upande wa utetezi na kumwakilisha Makamu wa rais wa Kenya William Ruto mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Mwingereza huyo pia alikuwa wakili wa upande wa utetezi wa rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor mbele ya Mahakama maalum ya Sierra Leone na wakili katika Mahakama Maalum ya Lebanon yenye makao yake huko Hague, iliyoundwa kwa minajili ya kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wauaji wa Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafic Hariri mnamo mwaka 2005.

ICC ina jumla ya wanachama 123 kati ya 193 wanaounda Umoja wa Mataifa. Marekani, Urusi, China, au hata Israeli, sio wanachama wa ICC. Muhula wa mwendesha mashtaka ni miaka tisa. Makao makuu ya ICC yanapatikana Hague. Karim Khan ambaye atakuwa mwendesha mashtaka wa tatu wa mahakama hii tangu kuundwa kwake mnamo mwaka 2002. Hata hivyo atakuwa na kibarua kigumu kwa kushughulikia kesi nyingi zenye utata, katika mahakama ambayo uhalali wake uko mashakani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.