Pata taarifa kuu
ZIMBABWE

Zimbabwe: Jeshi latangaza kumalizika kwa operesheni iliyomng'oa Mugabe

Mkuu wa majeshi nchini Zimbabwe ametangaza kumalizika kwa operesheni ya kijeshi iliyomlazimisha rais wa zamani Robert Mugabe kujiuzulu huku akitoa wito kwa wananchi kuwa watulivu kuruhusu mabadiliko ya Serikali.

Mkuu wa majeshi ya Zimbabwe, Costantino Chiwenga akihutubia waandishi wa habari mjini Harare hivi karibuni
Mkuu wa majeshi ya Zimbabwe, Costantino Chiwenga akihutubia waandishi wa habari mjini Harare hivi karibuni REUTERS/Philimon Bulawayo
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa jeshi la taifa Philip Valerio Sibanda amewaambia waandishi wa habari kuwa "Jeshi la ulinzi na usalama linakuja mbele yenu kutangaza kumalizika kwa operesheni ya kurejesha utawala thabiti".

"Hali ya kawaida imerejea nchini. Tunataka tuwashukuru wananchi wote wa Zimbabwe kwa kutuunga mkono, kuwa wavumilivu na waelewa katika kipindi cha majuma matano ya operesheni hii," alisema mkuu huyo wa jeshi la taifa.

Jeshi limewataka pia wananchi kuwa waangalifu nyakati zote na kutoa taarifa pale wanapoona shughuli zinazotia wasiwasi na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama.

Jeshi limesema kuwa linatoa wito huu kutokana na ukweli kuwa kundi lililokuwa likifahamika kama G40 lililokuwa limemzunguka rais Mugabe limeanza kuongea maneno mabaya kwa mataifa ya kigeni kwa lengo la kutatiza amani ya nchi hiyo.

Wanajeshi wakilinda jengo la bunge mjini Harare
Wanajeshi wakilinda jengo la bunge mjini Harare REUTERS/Philimon Bulawayo

Sibanda amesema kwa sasa wamerejesha mamlaka na madaraka yote ya ulinzi na usalama wa raia kwa jeshi la polisi.

Jeshi lilichukua hatamu ya kusimamia shughuli za nchi hiyo Novemba 15 mwaka huu wakati sintofahamu ilipoongezeka ndani ya chama tawala cha ZANU-PF kuhusu mrithi wa rais Mugabe.

Katika operesheni hiyo jeshi lilidai kuwa lilikuwa linawalenga washirika wa rais Mugabe ambao walikuwa wanajihusisha na rushwa hatua iliyokuja siku chache tu baada ya rais Mugabe kumfuta kazi aliyekuwa makamu wake wa rais na sasa ndiye rais Emmerson Mnangagwa aliyekuwa anapewa nafasi ya kumrithi.

Kuingilia kati huku kwa jeshi kulifuatiwa na maandamano ya nchi nzima kupinga utawala wa rais Mugabe na baadae kuwasilishwa kwa muswada kumundoa madarakani rais  ambaye baadae alimuandikia barua spika kumueleza kuwa amejiuzulu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.