Pata taarifa kuu

Tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria: idadi ya vifo sasa yazidi 30,000

Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba Uturuki na Syria siku sita zilizopita imeongezeka hadi zaidi ya 33,000 Jumapili Februari 12, huku msafara mpya wa Umoja wa Mataifa ukiwasili nchini Syria, na kuleta misaada kwa wahanga iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu.

Mwanamume mwenye umri wa miaka 23 ameokolewa kutoka chini ya vifusi huko Antakya, Uturuki Jumapili Februari 12.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 23 ameokolewa kutoka chini ya vifusi huko Antakya, Uturuki Jumapili Februari 12. AP - Petros Giannakouris
Matangazo ya kibiashara

Siku sita baada ya tetemeko la ardhi lililokumba Uturuki na Syria, idadi ya watu imeendelea kuongezeka. Kulingana na takwimu rasmi za hivi punde, ambazo bado ni za muda, tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 limeua watu wasiopungua 33,179 - 29,605 nchini Uturuki na 3,574 nchini Syria. Lakini kulingana na Umoja wa Mataifa, idadi ya waliofariki bado inaweza kufikia 'mara mbili'.

Nchini Uturuki, visa vya uokoaji wa kimiujiza mbali na kipindi muhimu cha saa 72 baada ya maafa vinaendelea kuripotiwa na wafanyakazi wa kutoa misaada wa Uturuki na vyombo vya habari. Huko Hatay, mwanamke mwenye umri wa miaka 63 alitolewa kwenye vifusi saa 158 baada ya tetemeko la ardhi. Huko Adiyaman, kijana mwingine mwenye umri wa miaka 23 aliokolewa saa 153 baada ya tetemeko hilo, saa moja baada ya dadake, mwalimu mwenye umri wa miaka 28, kuokolewa. Baba yao alifariki katika mkasa huo. Mwanamume mwenye umri wa miaka 35 aliokolewa saa 149 huko Hatay na askari wa jeshi la Uturuki na timu kutoka Italia na Romania, baada ya saa kumi na mbili za juhudi ambapo mwanamume huyo alikuwa akiimba chini ya vifusi kwa kujifariji.

Tishio

Takriban watu 32,000 sasa wamehamasishwa kwa shughuli za utafutaji na uokoaji nchini humo, pamoja na waokoaji zaidi ya 8,000 wa kigeni, kulingana na shirika la Uturuki linalohusika na majanga ya asili. Lakini baadhi ya timu za kimataifa za uokoaji bado zinakabiliwa na vitisho. Shirika lisilo la kiserikali la Israel United Hatzalah limetangaza siku ya Jumapili kusitisha shughuli zake kutokana na "tishio kubwa" kwa usalama wa timu yake kwenye eneo la tuko.

Siku ya Jumamosi, jeshi la Austria lilisimamisha shughuli zake za uokoaji kwa saa chache, likitaja "hali ya usalama". Mashirika matatu ya Ujerumani pia yalisitisha shughuli zao, kutokana na kuzorota kwa "hali ya usalama katika jimbo la Hatay", na "mapigano kati ya makundi tofauti".

Kwa upande wa Syria, ufikiaji wa maeneo yaliyoathiriwa ni ngumu zaidi kuliko Uturuki. Serikali ya Damascus siku ya Ijumaa iliidhinisha "kuwasilishwa kwa misaada ya kibinadamu kwa nchi nzima" - ikiwa ni pamoja na maeneo yanayoshikiliwa na waasi. 

Kwa mujibu wa afisa wa Wizara ya Uchukuzi ya Syria, Suleiman Khalil, ndege 62 zilizosheheni misaada hadi sasa zimetua nchini humo na nyingine zaidi zimetarajiwa katika saa na siku zijazo, hususan kutoka Saudi Arabia. Baada ya kutangaza kwa mara ya kwanza euro milioni 12.7 kama msaada wa kibinadamu kwa Syria, Umoja wa Falme za Kiarabu uliahidi msaada mpya wa euro milioni 47. Ishara iliyopokelewa na Rais Bashar al-Assad ambaye aliishukuru Abu Dhabi siku ya Jumapili kwa "msaada wake mkubwa wa kibinadamu". Kundi la Hezbollah nchini Lebanon, mshirika wa serikali ya Syria, kwa upande wake lilituma msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea magharibi mwa Syria, pamoja na 'chakula' na 'vifaa vya matibabu'.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.