Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Mashabiki ndani ya HF035 Air Cote d’Ivoire wakerwa kufungwa na Eq. Guinea 4-0

Abidjan, Cote D'Ivoire – Ni saa 5:10 jioni kwa saa za hapa San Pedro mojawapo ya miji inayoandaa Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2023. Nipo kwenye foleni ya ukaguzi wa kuabiri ndege aina ya HF035 Air Cote D'Ivoire inayoelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Feix Houphouet Boigny Abidjan kutoka uwanja wa ndege wa San Pedro.

Shabiki wa Cote d'Ivoire akihuzunikia matokeo ya timu pindi baada ya kushuka ndege uwanja wa Felix Houphouet Boigny jijini Abidjan
Shabiki wa Cote d'Ivoire akihuzunikia matokeo ya timu pindi baada ya kushuka ndege uwanja wa Felix Houphouet Boigny jijini Abidjan © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Ninapanga foleni kwa utulivu kushughulikia pasi yangu ya kuabiri lakini ili kujiweka bize kwa kuwa ni mpenda soka (sio tu kuwa kazi yangu) ninafuatilia mechi ya tatu ya Kundi A inayokutanisha wenyeji Cote D'Ivoire na Equatorial Guinea. Hadi sasa matokeo ni 0-0 na mashabiki wa Ivory Coast ambao pia wanasafiri nami wamevalia rangi zao za kitaifa (bendera, jezi, kofia na kadhalika). Wengi wao pia wanafuatilia mechi hiyo kwenye simu zao.

Kando yangu kuna duka la kubadilisha fulusi na mhudumu pia anafuatilia mechi kutoka Stade Alassane Ouattara huko Abidjan. Kandanda iko kwenye damu yao. Anaonekana kutatizika na kukosa subira akingojea nchi yake kufunga bao.

Ivory Coast inahitaji ushindi ili kukata tiketi ya moja kwa moja katika hatua ya mtoano au kufuzu kama moja ya timu zilizo nafasi ya tatu bora. Lakini hiyo ni njia ndefu kwa nchi mwenyeji kufuata, sivyo?

Dada mmoja nyuma yangu ananigusa bega na kuniuliza "matokeo yako vipi?" Jibu langu ni "0-0" ... "Ni kama tunachukua muda mrefu sana kupata bao!"

Mashabiki wa Ivory Coast kwenye uwanja wa ndege wa Abidjan
Mashabiki wa Ivory Coast kwenye uwanja wa ndege wa Abidjan © Jason Sagini

Dakika 40 baadaye, tunamaliza ukaguzi wetu wa usalama na sasa tuko katika eneo la kusubiri kuabiri ndege. Mchezo uko mapumziko. Lo! Kumbe tulikosa kushuhudia bao la Emilio Nsue tulipokuwa kwenye ukaguzi.

6:15pm ndege yetu inawasili. Tunakimbia haraka kukamilisha hatua ya mwisho kabla ya kupanda. 8B ndio kiti changu, tayari nimewasha simu yangu kutazama kipindi cha pili. Nimezungukwa na mashabiki wa Ivory Coast na wengine wa DRC katika viti vingine.

Wapo wanaulizana maswali "mechi ikoje?" Mmoja wa kina dada ananiuliza kwa kiingereza “Vipi matokeo na dakika ya ngapi?”

Mimi: Dakika 65, Eq. Guinea inaongoza 1-0.

Yule dada anageuka taratibu kwa kiti chake na kutulia tuli kama maji mtungini.

Dakika chache Jean Krasso anasawazisha mechi. Mashabiki wa Ivory Coast wanapata sauti hatimaye. Mmoja wao (wa kike) kwenye kiti cha mbele kabisa upande kuume anaamka na kuvalia jezi ya Wanatembo hao huku kwa sauti ya juu akisema “Yes, yes, yes!”

Nikiwa na mashabiki wa Cote d'Ivoire baada ya kutua uwanja wa ndege wa Felix Houphouet Boigy jijini Abidjan.
Nikiwa na mashabiki wa Cote d'Ivoire baada ya kutua uwanja wa ndege wa Felix Houphouet Boigy jijini Abidjan. © Jason Sagini

Ghafa bin vu, bao linakataliwa kwa kuwa Krasso alikuwa ameotea. Hili linashusha munkari wa yule shabiki wa kike na wengine wote. Wakati huu mashabiki wa DRC ni kicheko tu na kuwakejeli Ivory Coast.

Kabla ya ndege kupaa angani, Ivory Coast wanashambulia kwa presha ya juu bila mafanikio. Equatorial Guinea wanajibu kwa magoli mawili ya haraka, hili likipelekea kelele na kicheko cha mashabiki wa DRC kuongezeka. Ivory Coast ji!

6:30 jioni, ndege inaondoka na mtandao unakatika mechi ikiwa 3-0.

Safari ya kutoka San Pedro hadi Abidjan inachukuwa muda wa saa moja. Muda huu wote hatujui kinachoendelea uwanjani.

Ndege inapokaribia kutua, mimi huyo upesi nawasha mtandao wangu wa kuangalia matokeo.

Equatorial Guinea iliongeza bao moja na mechi kutamatika 4-0.

Bingwa mmoja tuliyekaa naye anawaambia wenzake matokeo kwa lugha ya kifaransa, kwa jinsi walivyoipokea, hakika ni taarifa iliyowakata maini. Kila mtu anaanza kutoa uchambuzi wake wa timu ya Cote d’Ivoire kwa ujumla.

“Siamini, ni kama ndoto isiyo ya kweli. Nakosa kuamini hata kama ni ukweli siwezi kukubali,” alisema shabiki wa Cote d’Ivoire (jinsia ya kike) kwa huzuni tena kwa sauti ya kutaka kulia.

Ama Ouattara alikiri ugumu wa kufuatilia mechi hiyo awali kupitia simu za watu waliokaa karibu yake na kutofautisha uvumi na ukweli wa matokeo halisi.

“Naaibika na nimekata tamaa kama mwanatembo sababu tunaandaa AFCON. Nilikuwa na matumaini zaidi, tuseme ukweli matokeo hayo ni ya kukatisha tamaa. Jiji limetulia, Hakuna kelele nje,” alisisitiza Ama.

Kufuatia matokeo hayo, Ivory Coast sasa inasubiri kila timu icheze mechi ya tatu ya makundi ili kuona ikiwa itafuzu kama mojawapo ya timu nne zitakazomaliza nafasi ya tatu kwenye makundi yao. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.