Pata taarifa kuu

Kenya kufuzu kombe la dunia 2026 itakuwa historia kubwa: Engin Firat

Nairobi – Na: Jason Sagini

Kocha wa Harambee Stars Engin Firat
Kocha wa Harambee Stars Engin Firat © Wizara ya michezo- Kenya
Matangazo ya kibiashara

Kocha wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars, Engin Firat amesema iwapo Kenya itafuzu fainali za kombe la dunia la mwaka 2026 itakuwa historia kubwa kwa taifa la Kenya. 

Firat alikuwa akizungumza kwenye kikao na wanahabari siku ya Jumatatu wiki hii jijini Nairobi nchini Kenya kabla ya kusafiri kuelekea jijini Franceville nchini Gabon kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Kundi F kufuzu michuano hiyo itakayoandaliwa nchini Marekani, Mexico na Canada. 

“Tuna imani kwa mwenyezi Mungu. Tutajaribu kadri ya uwezo wetu ila siwezi kutoa ahadi yoyote kwa sasa.” alisema kocha Engin Firat raia kutoka Uturuki. 

Wachezaji wa Kenya kwenye mazoezi uwanjani Kasarani Annex
Wachezaji wa Kenya kwenye mazoezi uwanjani Kasarani Annex © Wizara ya michezo- Kenya

Kenya itachuana na Gabon siku ya Alhamisi kabla ya kucheza na Ushelisheli siku ya Jumatatu wiki ijayo katika uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abidjan nchini Cote D’Ivoire. 

Kikosi cha Kenya hata hivyo kinakumbwa na majeraha si haba, wachezaji watano wa kikosi cha kwanza wakikosa kusafiri - mabeki Joseph Okumu (Reims, Ufaransa), Daniel Anyembe (Viborg, Denmark), Collins Shichenje (AIK, Uswidi), Brian Mandela (Mamelodi Sundowns, Afrika Kusini) na mlinda lango Bryne Odhiambo (KCB, Kenya).  

“Siwezi kulalamikia majeraha. Nina wachezaji wa kutosha na tuko tayari kupambana. Nimejaribu kuwaweka wachezaji pamoja ili kuwa tayari,” alisisitiza Firat. 

Beki wa Zanaco FC ya nchini Zambia, Dennis Ng’ang’a ndiye pekee aliitwa kikosini katika dakika za mwisho kujaza nafasi ya mabeki wazoefu wanaokosekana. 

Kikosi kamili cha timu ya taifa ya Kenya upande wa wanaume
Kikosi kamili cha timu ya taifa ya Kenya upande wa wanaume © Wizara ya michezo- Kenya

Kikosi cha mwisho alichoteua kocha Firat, kinajumuisha mabeki Nabi Kibunguchy (Orlando City, Marekani) na Haniff Wesonga (KCB, Kenya) ambao wameitwa kwa mara ya kwanza akimtema kiungo Erick Balecho (Murang’a Seal, Kenya), beki wa kushoto wa Gor Mahia Geoffrey Ochieng na mshambuliaji wa Kakamega Homeboyz ya nchini Kenya Moses Shummah. Firat pia aliamua kumshirikisha mfungaji bora hadi sasa wa ligi ya nyumbani Benson Omalla wa Gor Mahia baada ya kumweka pembeni kwa muda tangu mwezi Juni katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mauritius. 

Uchambuzi wa wapinzani 

Kwenye Kundi F, Gabon katika msimamo wa dunia wa FIFA, inaorodheshwa nafasi ya 86, Ivory Coast 52, Kenya 110, Gambia 117, Burundi 142 na Ushelisheli 195. 

“Tumejiandaa vizuri, tumecheza mechi nzuri za kirafiki ugenini na kupata matokeo mazuri. Gabon ni miongoni mwa timu bora Afrika, tunajua sifa zao, lakini hamna cha kuogopa,” alieleza nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga anayechezea Al Duhail SC nchini Saudi Arabia. 

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba akiwaaga wachezaji wa Harambee Stars
Waziri wa Michezo Ababu Namwamba akiwaaga wachezaji wa Harambee Stars © Wizara ya michezo- kenya

Kocha mpya wa Gabon Thierry Mouyouma hajamjumuisha mshambuliaji mahiri na mfungaji bora wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang (mabao 30) kwenye kikosi chake ila kikosi hicho kinajivunia nyota kama vile mfungaji bora wa ligi ya Marekani Dennis Bouanga, mfungaji bora wa ligi kuu ya Uturuki mwaka 2021 Aaron Boupenza na mchezaji wa Wolves ya Uiingereza Mario Lemina pamoja na mabeki kadhaa wanaocheza ligi kuu ya soka nchini Italia na Ufaransa. 

Wema hutuzwa 

Timu ya Kenya imeondoka leo asubuhi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, ikisindikizwa na waziri wa masuala ya vijana na michezo nchini Kenya, Ababu Namwamba.  

 “Serikali imeweka juhudi zote kuhakikisha maandalizi sahihi kwa ajili yenu. Tayari tumelipa marupurupu yenu na kukodisha ndege hii ili tupunguze uchovu wa ndege. Nina imani na kikosi hiki na ninawahimiza mujitolee muwezavyo,” alisema waziri Ababu. 

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba akiipungia kwaheri ndege iliyobeba timu ya taifa Harambee Stars
Waziri wa Michezo Ababu Namwamba akiipungia kwaheri ndege iliyobeba timu ya taifa Harambee Stars © Wizara ya michezo- Kenya

Waziri Ababu ametoa ahadi ya milioni 2.5 pesa za Kenya ($16.4/ €15.1) kwa kila alamu tatu watakazozipata kwenye mechi hizo za kufuzu Kombe la Dunia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.