Pata taarifa kuu

Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kwa muda ukarabati ukiendelea

NAIROBI – Na Paul Nzioki

Uwanja wa kimataifa wa michezo nchini Tanzania
Uwanja wa kimataifa wa michezo nchini Tanzania © CAF
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya jamhuri ya muungano ya Tanzania imetangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kutoa nafasi ya kufanyiwa ukarabati.

Timu ya taifa ya Tanzania imeratibiwa kucheza dhidi ya Niger katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

Taifa Stars itamenyana na Niger katika uwanja huo mjini Dar es Salaam Juni 17 katika kundi F kabla ya kwenda Algiers kumenyana na Algeria Septemba 4.

Vijana hao wa Tanzania wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi F wakiwa na alama nne sawa na majirani wao Uganda walio katika nafasi ya tatu huku Niger ikiwa mkiani ikiwa na alama mbili.

Algeria wapo kileleni wakiwa na pointi 12 na tayari wamefuzu kwa fainali za Afcon zitakazofanyika nchini Ivory Coast.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Algeria
Wachezaji wa timu ya taifa ya Algeria BackpagePix - Gavin Barker/BackpagePix

Akizungumza wakati wa kuwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana amesema uwanja huo unahitaji marekebisho makubwa ili kuboresha kiwango chake.

Chana ameeleza kuwa watashirikiana na wadau wa soka kukarabati uwanja huo.

“Tutaufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa mara baada ya timu yetu ya Taifa (Taifa Stars) kucheza dhidi ya Niger katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON, tulikuwa na kamati ambayo ilipitia hali ya uwanja huo na ikatoa ripoti kuwa unahitaji kufanyiwa ukarabati kwa utaratibu. ili kurudisha hadhi yake ya awali,” alisema Chana.

Kwa mujibu wa waziri chana, serikali pia itajenga viwanja viwili vya kisasa vya michezo mjini Dodoma na Arusha.

Waziri aliongeza kuwa viwanja vitakavyojengwa viko katika mipango yao ya kuandaa fainali za Afcon mwaka 2027 pamoja na Uganda na Kenya.

Mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania yanataka kuwa mwenyeji wa AFCON 2027
Mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania yanataka kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 © State House Kenya

"Katika kuandaa fainali za Afcon, unahitaji kuwa na viwanja vya kisasa visivyopungua vinane. Kwa kuwa tuko na Kenya na Uganda, tuna uhakika wa kushinda zabuni na viwanja viwili vitakuwa tayari kabla ya fainali za 2027," alisema.

Kwa mujibu wa Chana, Baraza la Michezo la Taifa Tanzania (BMT) linatarajia kukusanya Sh920 milioni katika mwaka ujao wa fedha, kinyume na Sh685 milioni zilizotarajiwa kukusanywa katika mwaka wa fedha uliopita.

Tanzania itacheza mechi ya kufuzu  AFCON dhidi ya Niger
Tanzania itacheza mechi ya kufuzu AFCON dhidi ya Niger SuperSport

"Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Michezo, inatarajia kukusanya Sh1 bilioni kutoka kwa viingilio vya michezo mbalimbali na kukodisha uwanja wa mazoezi," alisema.

Bajeti ya mwaka ujao wa fedha nchini Tanzania, wizara hiyo pia imebainisha kuwa Sh1.12 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Dar es Salaam huku Sh130 milioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo na Sanaa.

“Serikali itaendelea kusaidia michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwezesha timu mbalimbali za Taifa,” alisema Waziri. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.