Pata taarifa kuu

Utayari wa nchi za Afrika Mashariki kuandaa AFCON 2027

NAIROBI – Na Mchambuzi wetu Jason Sagini

Nchi za Afrika Mashariki zimetuma ombi la kuaanda mechi za AFCON
Nchi za Afrika Mashariki zimetuma ombi la kuaanda mechi za AFCON SuperSport
Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita shirikisho la mpira barani Afrika, CAF, lilitangaza kupokea rasmi ombi la pamoja kwa mataifa ya Afrika Mashariki kuandaa kombe la mataifa ya Afrika ya mwaka 2027. Algeria, Botswana na Egypt ni miongoni mwa mataifa mengine ambayo tayari yamewasilisha nia ya kuandaa michuano hiyo.

Misri iliandaa mashindano ya mwaka 2019 wakati Algeria iliandaa mashindano ya mwaka huu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani maarufu CHAN pamoja na kuandaa mashindano ya wachezaji wasiozidi miaka 17. Hii ikiwa na maana kuwa mataifa haya mawili hayana changamoto ya miundo misingi bora ya kuandaa michuano.

Hadi kufikia wiki jana, Botswana ilifaa kuwasilisha ombi la pamoja ila Namibia ikajiondoa dakika za mwisho kutokana na changamoto za kifedha. Hata hivyo, haijulikani ni kiasi gani cha uwekezaji kitahitajika kuruhusu aidha ya Botswana au nia ya pamoja ya Afrika Mashariki kufanikiwa kupewa jukumu la kuandaa mashindano ya mwaka 2027.

Algeria waliaandaa mashindano ya CHAN 2023.
Algeria waliaandaa mashindano ya CHAN 2023. REUTERS - RAMZI BOUDINA

Utayari na uwezo wa nchi za Afrika Mashariki kuandaa mashindano haya makubwa ya soka

Hadi kufikia mwaka 2021, Kenya ilikuwa na uwanja mmoja tu ulioidhinishwa na CAF kuandaa mechi za kimataifa- uwanja wa Nyayo. Licha ya kuwa uwanja wa Moi Kasarani unamiliki jina la kimataifa, CAF ilisema hapo awali kuwa haukuwa umeaafikia viwango vya kuandaa mechi za kimataifa.

Kenya ilipokonywa haki za kuandaa mashindano ya CHAN 2018 miezi minne tu kabla ya fainali hizo kwa sababu viwanja kadhaa havikuwa tayari. Kenya pia iliwahi kupokonywa haki za kuandaa kombe la mataifa ya Afrika ya mwaka 1996 kutokana na sababu hizo. Shirikisho la mpira wa miguu nchini Kenya kupitia wizara ya michezo inayoongozwa na waziri Ababu Namwamba wanalenga viwanja vyao viwili kuidhinishwa kabla ya ukaguzi kufanywa na CAF.

Waziri wa michezo nchini Kenya Ababu Namwamba
Waziri wa michezo nchini Kenya Ababu Namwamba © Ababu Namwamba

Nchini Tanzania, uwanja wa Benjamin Mkapa ndio uwanja pekee wenye viwango vya kimataifa na umeandaa mechi kadhaa za Simba SC na Young Africans kwenye mashindano ya vilabu barani Afrika. Ila uwanja huo unakabiliwa na tatizo la umeme. Suala ambalo limekuwepo kwa muda sasa.

Mwezi Machi tarehe 28 katika mechi ya timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Uganda kufuzu kombe la mataifa ya Afrika 2023, umeme ulikatika uwanjani katika dakika 38. Taa hizo zilionekana kupungua mwanga, baadhi yake zikazima kabisa hata baada ya ukarabati nyingine hazikuwaka kabisa. Hili lilijirudia majuzi tarehe 30 mwezi Mei mwaka 2023, katika mchezo wa kombe la shirikisho mkondo wa pili kati ya Yanga na Rivers United ya Nigeria wakati taa zilizima ghafla kipindi cha kwanza dakika ya 24.

Taa zilizima katika uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania wakati wa mechi ya shirikisho kati ya Young Africans  dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria
Taa zilizima katika uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania wakati wa mechi ya shirikisho kati ya Young Africans dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria © Courtesy of CAF

Taifa la Uganda nalo pia linakumbwa na matatizo ya viwanja kwani nchini humo, hakuna uwanja ulioidhinishwa na CAF kuchezesha mechi za kimataifa. Mechi ya nyumbani ya timu ya taifa Uganda Cranes dhidi ya Tanzania kuwania kufuzu kombe la mataifa ya Afrika ya mwaka 2023 ilichezwa nchini Misri kutokana marufuku ya Caf kwa viwanja vya Uganda. Uwanja wa Nelson Mandela ndio uwanja mkubwa nchini Uganda wenye uwezo wa kubeba mashabiki zaidi ya elfu 45 ukifuatiwa na uwanja wa St. Mary’s Kitende ambao hivi majuzi uliwekwa taa na hivyo basi kuwa na uwezo wa kuchezesha mechi za usiku.

Mashabiki wa Uganda, ambao timu yao imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza kombe la mataifa ya Afrika kule Gabon mwaka ujao.
Mashabiki wa Uganda, ambao timu yao imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza kombe la mataifa ya Afrika kule Gabon mwaka ujao. Fufa.com

Iwapo CAF itaidhinisha ombi la mataifa ya Afrika Mashariki, bado kuna muda wa miaka mitatu kurekebisha hali ya viwanja. Tayari katibu mkuu wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Saidi Yakubu amesema mikataba mitatu ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa itasainiwa mwaka huu ili kuhakikisha unakuwa bora zaidi. Maeneo yatakayofanyiwa ukarabati ni nyasi, vyumba vya wachezaji pamoja na maeneo ya kukaa wanahabari na watu mashuhuri.

Umuhimu upo wa serikali hizi tatu kupitia wizara za michezo kushirikiana ili kuboresha hali za viwanja kabla ya ukaguzi kufanywa.

Rais wa CAF, Patrice Motsepe
Rais wa CAF, Patrice Motsepe © Pierre René-Worms

CAF itatangaza mshindi wa kuandaa mashindano ya 2027 mwezi Septemba pamoja pia na waandalizi wa mashindano ya mwaka 2025 baada ya Guinea kupokonywa haki za kuandaa mwezi Oktoba mwaka jana kutokana na maandalizi duni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.