Waamuzi wa michuano ya robo fainali klabu bingwa na Shirikisho wafahamika
NAIROBI – Na Mchambuzi wetu Paul Nzioki
Imechapishwa:
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limemteua mwamuzi kutoka taifa la CHAD Alhadi Allaou Mahamat kuchezesha mchezo kati ya Simba SC ya Tanzania na Wydad Club Athletic ya Morocco.
Mechi hii itakua ya mkondo wa pili katika mechi za kuwania ubingwa wa vilabu barani Afrika.
Simba itashuka dimbani kesho Jumamosi saa tisa alasiri kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V (Maarufu Mohammed Wa Tano) mjini Casablanca, Morocco.
Simba ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa (Maarufu Estadio De Benjamin Mkapa) jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Simba itakosa huduma za wachezaji wake watatu, Mlinda lango Aishi Manula ambaye anauguza jeraha , Augustine Okrah na Mohamed Ouattara.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo maarufu kama Robertinho, alisema wataenda kuthibitisha thamani yao katika pambano hilo licha ya kukabiliwa na kibarua kigumu.
Wakati huo huo, mchezo wa marudiano wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na Rivers United, utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Redouane Jiyed atakuwa katikati ya uwanja katika pambano hilo ngumu.
Young Africans wanahitaji sare yoyote ili kuweka historia ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo na wao pia kuvunja mwiko wa timu za Tanzania kutoshiriki hadi nusu fainali katika michuano ya CAF.
Wananchi walipata ushindi wa 2-0 ugenini katika uwanja wa Goodwill Akpabio kule Nigeria.
Wachezaji wa Yanga wameanza mazoezi jana kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 7 mchana Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.