Pata taarifa kuu

Kenya inajipanga kupigana na visa vya dawa za kututumua misuli

NAIROBI – Na Jason Sagini

Nembo ya shirika la kupambana na dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo duniani WADA
Nembo ya shirika la kupambana na dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo duniani WADA AFP
Matangazo ya kibiashara

Kamati ya kupambana na utumiaji wa  dawa zinazoongeza nguvu mwilini kwa wanamichezo nchini Kenya kwa ushirikiano na shirika la ADAK, kitengo cha uadilifu cha riadha duniani na shirikisho la riadha nchini humo, limetoa ripoti ya namna ya kupambana na changamoto hiyo.

Hii ni baada ya ziara ya wajumbe wa shirikisho la riadha duniani likiongozwa na rais Sebastian Coe kuzuru taifa la Kenya mapema mwaka huu mwezi Januari. 

Waziri wa michezo nchini Kenya Ababu Namwamba amesisitiza mara kwa mara kwenye mikutano kadha aliyopanga ya kujadili swala hili kuwa ni mojawapo ya malengo yake kuu ya kutendea kazi ofisini.

Kitengo cha uadilifu cha riadha duniani lilisema ukosefu wa mikakati ya kuwalinda wanariadha inatengeneza mazingira rafiki ya visa hivyo kuongezeka. 

Nembo ya shirika la kupambana na dawa za kuongeza nguvu mwilini kwa wanamichezo, WADA
Nembo ya shirika la kupambana na dawa za kuongeza nguvu mwilini kwa wanamichezo, WADA AFP

Mkurugenzi mkuu wa kitengo hicho Brett Clothier amesema kuna ukimya wa  takriban wanariadha wote wa Kenya ambao wamepigwa marufuku kwa kutumia dawa za kusisimua misuli kwa kuhofia wahalifu wanaohusika na upangaji wa dawa hizo.

Kenya imeorodhoshewa kwenye orodha ya nchi zenye ongezeko la visa vya ututumuaji misuli duniani tangu mwaka 2015. Baadaye mwaka 2016 mamlaka inayozuia matumizi ya dawa za kututumua misuli iliundwa ili kupambana kuinasua Kenya katika kitengo hicho. 

Hadi sasa zaidi ya wanariadha 200 wamepigwa marufuku kutoka nchini Kenya. Kisa cha kwanza nchini Kenya kiliripotiwa mwezi Februari mwaka 1988 na cha pili mwaka 1992. Purity Changwony anayeshiriki mbio za masafa marefu ndiye wa hivi punde kupigwa marufuku. 

Olimpiki Paris mwaka wa 2024
Olimpiki Paris mwaka wa 2024 © Michel Euler / AP

Alice Jepkemboi Kimutai na Johnstone Kibet Maiyo pia walipokea adhabu ya miaka mitatu mwezi Desemba mwaka 2022 wakati Mark Otieno anayeshiriki mbio za mita 100 alipokea adhabu ya miaka miwili wakati wa mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2020 huko Tokyo, Japan miongoni mwa wengine wengi.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi za waziri wa michezo nchini Kenya, rais wa shirikisho la riadha Jackson Tuwei, alitoa maelezo ya mikakati waliokubaliana.

“Tutazingatia zaidi jinsi ya kuendesha shughuli ya vipimo kwa wanariada wetu na pia kubaini majukumu ya kila mmoja wetu.” alisema Jackson Tuwei

Katika ripoti hiyo vipimo hivyo na uchunguzi vitafanyika mara kwa mara ili kuweka rekodi ya kila mwanariadha kabla na baada ya mashindano pamoja pia na kutumia wanasaikolojia katika visa vya dhuluma ya kijinsia. Pia mamlaka hiyo imeratibu kuanzishwa kwa mafunzo kwa wanariadha, wanahabari na umma kuhusu visa vya kutumia dawa za kututumua misuli.

“Idara zote hizo zimeanzishwa, na leo tulikua tunawasilisha ripoti hii kwa waziri wa michezo na ikipitishwa baada ya serikali kutenga fedha za ufadhili, tutapiga hatua moja kwa moja katika utekelezwaji,” alisisitiza Jackson Tuwei.

Akipokea ripoti hiyo kwa niaba ya waziri wa michezo, katibu mkuu katika wizara hiyo Jonathan Mueke alikuwa mwingi wa matumaini ya kurejesha hadhi ya taifa la Kenya kwenye riadha.

“Naamini kuwa mpango huo ukitekelezwa jinsi ulivyopangwa basi hamtasikia suala hili tena hapa nchini Kenya na najua hivi karibuni tutarejea kwa kishindo kikubwa. Tunajitolea kwa hali na mali kama serikali kuhakikisha wanariadha wetu wanazidi kupeperusha bendera ya taifa duniani bila kujihusisha na udanganyifu kwenye michezo,” alisisitiza katibu mkuu wa michezo, Jonathan Mueke.

Ripoti hiyo inatarajiwa kuchapishwa wazi kwa umma hivi karibuni.

Mkurugenzi mkuu wa kitengo cha uadilifu cha riadha duniani Brett Clothier alisifia hatua ya serikali ya Kenya kutenga dola milioni tano kila mwaka kwa miaka mitano ijayo kama ufadhili wa kupambana na visa vya ulaji muku. Aidha Clothier alionya kuwa visa hivyo vitaongezeka kwa miezi michache ijayo baada ya kuongeza idadi ya vipimo kama walivyopa,nga kwenye ripoti yao.

“Uchunguzi wetu kwa watu wanaohusika katika visa hivyo pia vitaongezeka,” alisema Clothier.
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.