Pata taarifa kuu
MATUKIO 2023

Matukio makubwa ya michezo yatakayojiri mwaka 2023

Mwaka mpya na mambo mapya. Bila shaka viwanjani pia tunatarajia mbwembwe mpya kama tuliyoshuhudia mwaka jana (2022). Makala haya yanaangazia matukio makubwa ya kispoti ya mwaka 2023 ambayo kila shabiki wa michezo anasubiria kwa hamu na ghamu.

Mpira wa miguu
Mpira wa miguu © AFP - SEBASTIEN BOZON
Matangazo ya kibiashara
Mashindano ya CHAN yatakayoanza Januari 13 hadi Februari 04 nchini Algeria.
Mashindano ya CHAN yatakayoanza Januari 13 hadi Februari 04 nchini Algeria. © CAF on line

Mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani yatang’oa nanga tarehe 13 Januari na kukamilika Februari 4 nchini Algeria. Morocco ndio mabingwa watetezi baada ya kushinda taji lao la pili mwaka 2020, mara ya kwanza ikiwa 2018.

DR Congo na Morocco ndio timu pekee kuwahi kushinda taji hilo mara nyingi (2). Makala ya mwaka huu yana mgeni mmoja tu Madagascar. La kusubiriwa ni ikiwa Morocco ambao walikuwa na mafinikio makubwa mwaka 2022, kama neema hiyo itawafuata na kuweka historia kwa kunyakua kombe hili mara tatu mfululizo.

FIFA Club World Cup 2023

Kwa mara ya kwanza kabisa, mashindano ya klabu bingwa duniani yataandaliwa katika ardhi ya Afrika – nchini Morocco kuanzia Februari 1-11. Vilabu vitakavyoshiriki ni; mabingwa wa bara Afrika Wydad Casablanca, Al Ahly ya Misri, mabingwa wa bara Ulaya Real Madrid, mabingwa wa bara Amerika Flamengo, Al Hilal ya Saudi Arabia, Seattle Sounders ya Marekani na Auckland City ya New Zealand.

Kama tu kwenye CHAN, macho mengi yatamulika Wydad ya Morocco ila pia Al Ahly ambao wamemaliza nafasi ya tatu katika makala tatu yaliyopita mwaka 2006, 2020 na 2021.

Kombe la Dunia la kriketi kwa kina dada

Afrika Kusini ndio waandalizi wa toleo la nane la kombe la dunia la kriketi kwa kina dada kuanzia tarehe 10 Februari hadi 26. Ni kombe ambalo lilianzishwa mwaka 2009 na taifa la Australia limetawala sana mashindano haya kwa kushinda vikombe tano ambayo ni historia kwa kuwa taifa lenye mafanikio zaidi kwenye mashindano.

Tour du Rwanda

Jean Bosco Nsengimana mshindi wa mashindano ya mwaka 2015
Jean Bosco Nsengimana mshindi wa mashindano ya mwaka 2015 Christophe Jousset

Mashindano ya baiskeli ambayo hufanyika kila mwaka nchini Rwanda yataandaliwa kuanzia tarehe 19 Februari hadi 26. Raia wa Eritrea Natnael Tesfatsion alishinda mashindano ya mwaka jana, mnyarwanda Eric Manizabayo alimaliza nafasi ya tisa ila mwenzake Moise Mugisha alijvunia kushinda hatua ya mwisho na kutajwa mshindi wa kitengo cha milima na mabonde.

Rwanda ilitawala mashindano haya kwa misimu mwili – kutoka 1998-2005 na 2014-2018. Mnyarwanda wa mwisho kushinda Tour du Rwanda ni Samuel Mugisha mwaka 2018. Tangu wakati huo raia wa Eritrea wawili wameshinda na mhispania mmoja. Bila shaka nina imani kuwa shirikisho la mchezo wa baiskeli nchini Rwanda (FERWACY) linajiandaa kuhakikisha kuwa taji halichukuliwi na wageni tena.

AFCON U20

Kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wasiozidi miaka ishirini litaandaliwa nchini Misri kuanzia Februari 19 hadi Machi 11. Unazikumbuka Comoros na Gambia kwenye AFCON 2021 nchini Cameroon? Walikuwa washiriki kwa mara ya kwanza na waliwashangaza wengi kwa kufika kwenye hatua ya muondoano.

Sudan kusini ambao ni washiriki kwa mara ya kwanza pia ni timu ya kuangaziwa. Sudan kusini ilipoteza kwenye fainali ya CECAFA dhidi ya Uganda – kiashiria tosha cha uwezo wao wa kufika mbali pasipotarajiwa.

Tour du France

Mashindano ya mwaka huu ya uendeshaji baiskeli nchini Ufaransa kwa wanaume yataanza tarehe moja Juni hadi tarehe 23 na tarehe 23 hadi 30 kwa mashindano ya kina dada ambayo yatakuwa makala ya pili tangu kubuniwa.

Tennis

Bingwa wa Wimbeledon mwaka 2022 Novak Djokovic kutoka Serbia
Bingwa wa Wimbeledon mwaka 2022 Novak Djokovic kutoka Serbia REUTERS - TOBY MELVILLE

 

Mashindano ya tenisi ya Wimbledon ndio mashindano kongwe zaidi duniani na taji lenye hadhi ya juu zaidi. Wimbledon ni mojawapo ya taji nne za Grand Slam pamoja na Australian Open, French Open, na US Open.

Wimbledon ndio mashindano pekee ya tenisi ambayo bado huchezwa kwenye nyasi.

Novak Djokovic ndiye bingwa mtetezi ameshinda Grand Slam 21 na atafukuzia kuweka rekodi sawa na ya Rafael Nadal ya Grand Slam 22. Ila muhispania Carlos Alcaraz mwenye miaka 19 ni chipukizi mwenye uwezo mkubwa. Kwa sasa ndiye anayeshikilia nafasi ya kwanza duniani baada ya kushinda US Open mwaka 2022. Aliweka historia kuwa mchezaji mchanga zaidi kushinda shindano la tenisi. Wengine pia ni kama vile Casper Ruud.

Wimbledon itaandaliwa kati ya tarehe 3-16 mwezi Julai.

Kombe la Dunia la kina dada mchezo wa soka

Baada ya kushuhudia Argentina wakishinda taji lao la tatu la dunia nchini Qatar, mashabiki wa soka tena wana nafasi ya kutazama kombe la dunia kwa kina dada litakaloandaliwa nchini Australia na New Zealand kuanzia Julai 20 hadi Agosti 20.

Kikubwa ni kusubiri kuona ikiwa Ufaransa itaboresha matokeo ya mwaka 2011 walipomaliza nafasi ya nne baada ya kushiriki mara tano tangu mwaka 2003. Wapo kwenye kundi moja na Jamaica na Brazil.

Afrika itawakilishwa na mabingwa bara Afrika, Afrika Kusini kwenye kundi moja na Uswidi, Italia na Argentina. Nigeria ambao walifika robo fainali ya mwaka 1999 na ni washindi wa bara afrika mara 11 wapo kwenye kundi moja na Australia, jamhuri ya Ireland na Canada. Zambia ambao ni washindi wa mwisho wa medali ya shaba kwenye kombe la bara Afrika wapo kwenye kundi moja na Japan, Cost Rica na Uhispania. Morocco watapambana na Ujerumani, Colombia na Korea Kusini. Mojawapo kati ya Cameroon na Senegal bado ina nafasi ya kufuzu kwenye hatua ya mwisho. 

Kombe la Dunia - Netiboli

Toleo la kumi na sita la kombe la dunia la netiboli litaandaliwa nchini Afrika Kusini kati ya tarehe 28 Julai hadi Agosti 6 ambapo New Zealand mabingwa mara tano watalenga kuutetea ubingwa wao walioushinda mwaka 2019. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa muondoano mwaka 1991, fainali sita kati ya nane ziizochezwa zimekuwa kati ya New Zealand na Australia ambao wameshinda kombe hili mara nyingi zaidi (11). Ni jambo la kusubiri kuona kama wawili hao watakutana tena kwenye fainali wakati wenyeji watalenga kuboresha matokeo ya mwaka 1995 walipomaliza nafasi ya pili kwa kulazwa na Australia kwenye fainali.

Michezo ya Afrika (All Africa Games)

Bila shaka Kenya na Ethiopia zitatarajiwa kupeperusha bendera ya Afrika mashariki ifikapo tarehe nne Agosti jijini Accra, Ghana. Kwenye orodha ya medali tangu kuasisiwa kwa mashindano, Kenya inashikilia nafasi ya sita kwa jumla ya medali 442. Katika makala ya mwaka 2019 jijini Rabat, Morocco, Kenya ilinyakua medali 31 – medali moja chini ya walizoshinda (32) mwaka 2015 jijini Brazzaville, Congo

Mashindano ya Riadha ya dunia

Mwanariadha wa Ethiopia Letesenbet Gidey aliposhinda mbio za Mita 10 000 wakati wa mashindano ya riadha ya dunia mjini   Eugene (Oregon), Julai 2022.
Mwanariadha wa Ethiopia Letesenbet Gidey aliposhinda mbio za Mita 10 000 wakati wa mashindano ya riadha ya dunia mjini Eugene (Oregon), Julai 2022. REUTERS - LUCY NICHOLSON

Kwenye mashindano ya riadha ya dunia ya mwaka jana jijini Oregon Marekani, Kenya na Ethiopia zilishinda medali 10 kila mmoja na kuorodheshwa kwenye kibano cha tano bora. Kenya ambayo ilishinda mashindano ya mwaka 2015 jijini Beijing, inashikilia nafasi ya pili kwenye orodha ya medali tangu mashindano kuasisiwa – medali 161 nyuma ya Marekani (medali 414).

Tutasubiri tuone ikiwa Marekani itaendelea kutawala mashindano haya baada ya kushinda mara kumi nne kati ya mashindano 18 ikiwemo ushindi kwenye makala tatu yaliyopita.

Mashindano yataandaliwa Budapest nchini Hungary kati ya tarehe 19-27 mwezi wa Agosti.

Kombe la Dunia la raga kwa wanaume

Ufaransa ndio wenyeji wa kombe la dunia la raga kwa wanaume kuanzia tarehe nane Septemba hadi 28 Oktoba. Afrika kusini ndio mabingwa watetezi na washindi mara tatu wa kombe hilo. Mashabiki kwenye ukanda wa afrika mashariki watasubiri sana kuona Namibia ambayo iliibandua Kenya itafika hatua gani kwenye mashindano.

Kombe la dunia la wanaume – Kriketi

New Zealand wamekuwa na mikosi kwenye fainali mbili za mwisho haswa fainali ya 2019 walipopoteza kupitia muda wa ziada yaani (boundary countback after a super over) dhidi ya Uingereza. Mwaka 2015 walipoteza kwenye fainali dhidi ya Australia kupitia wiketi saba.

Tangu kuanzishwa kwa kombe la dunia la kriketi mwaka 1975, mshindi hajawahi kubainika kupitia muda wa ziada bali njia ya wiketi (wickets) au mikimbio (runs). Fainali yam waka 2019 ilikuwa ya kwanza kuhitaji muda wa ziada kubaini mshindi.

Tusubiri ifikapo mwezi Oktoba nchini India, tutajua ikiwa Australia itaepuka mkosi wa fainali au tena tutashuhudia njia ya super over kutumika kubaini mshindi.

Formula One

Msimu mpya wa mchezo wa uendeshaji magari yaani langalanga, utaanza tarehe tano mwezi Machi na kukamilika tarehe 26 Novemba. Kikubwa cha kusubiriwa ni bingwa mara saba Lewis Hamilton kutia saini kandarasi mpya na timu yake ya Mercedes kabla ya kupambana na Max Verstappen wa Red Bull ambaye ameshinda taji mbili mfululizo – 2021 na 2022.

Lewis alishinda mikondo tano pekee msimu jana na kumaliza katika nafasi ya sita. Je Max ataendeleza rekodi yake nzuri msimu ujao?

Fainali za ligi ya mabingwa barani Afrika na Ulaya

Wachezaji wa klabu ya Wydad Casablanca, wakisheherekea ushindi wa klabu bingwa barani Afrika mwaka 2022
Wachezaji wa klabu ya Wydad Casablanca, wakisheherekea ushindi wa klabu bingwa barani Afrika mwaka 2022 © AFP - -

Real Madrid na Wydad Casablanca zitafukuzia kutetea ubingwa wao kwenye ngazi ya klabu bingwa. Tutasubiri sana kuona kocha mpya wa Simba Roberto Olivieira atakapowafikisha ‘wekundu wa msimbazi’ haswa baada ya kuiongoza Vipers ya Uganda msimu jana kufika hatua ya makundi kwa mara kwanza kabisa kwa kuilaza TP Mazembe nchini DR Congo. Vipers na Simba zipo kwenye kundi moja. Washindi wa mwaka 1973, AS Vita Club kutoka DR Congo wapo kwenye kundi moja na Petro Atletico ya Angola, JS Kabylie ya Algeria na Wydada Casablanca ya Morocco

Kocha Pep Guardiola hatimaye alimnasa mshambulizi Erling Haaland ambaye anafunga magoli kama inavyostahili kwa straika. Kwa hivyo wengi watasubiri kuona ikiwa Manchester City itafanikiwa kushinda kombe la bara Ulaya ambalo Pep anamezea mate sana.

Kama tu Man City, PSG ya Ufaransa nayo safari hii italenga kuepuka nuksi kwenye ligi hii wakicheza mara kwa mara bila kushinda taji. Kwa sasa ushindi wa kombe la dunia kwa Messi na umahiri wa Mbappe na Neymar ni sharti uwe nguzo muhimu kunyakua ubingwa huu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.