Pata taarifa kuu
KOMBE LA DUNIA 2022

Uchambuzi: Makocha walio kwenye hatari ya kufutwa kazi kuelekea kombe la Dunia

Na:Mchambuzi wetu, Jason Sagini

Kombe la dunia, Qatar 2022
Kombe la dunia, Qatar 2022 © Shutterstock
Matangazo ya kibiashara

Harusi bila keki haitaitwa harusi sawa na mechi ya soka bila magoli haishabikiwi. Mchezo huu kwenye karne ya sasa umebadilika sana.

Mashabiki wanapotaka soka ya kuvutia vilevile wanataka matokeo ya alama tatu kwa kila mechi. Kwa hivyo, makocha wenye sifa za kuwatia moyo wachezaji hawashabikiwi sana siku hizi bali wenye mbinu wamechukua nafasi hizo.

Hatuwezi wakosea heshima makocha hao ila kulingana na vipaji kwenye vikosi vyao ni sharti wazalishe matokeo bora sababu si kila miaka utapata vipaji kama hivyo.

Kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez
Kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez AFP

Ubelgiji chini ya mwalimu Roberto Martinez - wana timu nzuri sana na yenye vipaji vya kutosha ambazo ziliwawezesha kusalia kileleni mwa jedwali la FIFA kwa miaka mitatu tangu Septemba 2018 ila swali linabaki moja tu je wameshinda mataji mangapi tangu mwaka huo? Je ndiye kocha sahihi kwenye benchi la ufundi mwenye uwezo wa kutumia vipaji hivyo kutwaa mataji? Je, Martinez anatosha kuelekea Qatar? Napinga.

Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps.
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps. AFP - FRANCK FIFE

Didier Deschamps mwalimu wa Ufaransa ana kikosi kizuri na vipaji vichanga. Wao wanapiga soka ya madoido yenye kuvutia. Ukiwa uwanjani kwa mechi ya Ufaransa utapokea burudani kamili kutokana na chenga za Kylian Mbappe, Ousmane Dembele, pasi bunifu za kiungo wa kati Paul Pogba na kiungo kisiki Ngolo Kante.

Usisahau ndio mabingwa wa dunia kutokana na vipaji hivyo. Kwenye michuano ya ligi ya mataifa ya ulaya, Ufaransa iliponea kushushwa daraja kutoka ligi A licha ya kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Denmark Jumatatu usiku – Denmark ambayo watakutana tena kwenye kombe la dunia.

Kwa nini utumie mabeki watano wakati una mawinga – Dembele, Nkunku - wenye kasi kwenye benchi? Kwa nini umtumie Wesley Fofana kama kiungo wa kati wakati una Eduardo Camavinga na Matteo Guendouzi kwenye benchi? Najua wengi mtasema kocha Didier, anawakosa sana Pogba na Kante kwenye kiungo cha kati kwa sababu ya majeraha lakini tufahamu kuwa Camavinga na Tchouameni hawawezi kucheza pamoja na kuzalisha matokeo mazuri sababu wote ni kinda.

Kocha ana kazi kubwa kubaini nani mzoefu atamuita kikosini ili kujaza pengo la Pogba na Kante kama hawatakuwa wametoka mkekani. Pia usisahau historia ya bingwa mtetezi kwenye kombe la dunia. Unakumbuka Uhispania kwenye mashindano ya 2014 walibanduliwa hatua ya makundi sawa na Ujerumani kwenye mashindano ya 2018 walimaliza wa mwisho kwenye kundi lao.

Shirikisho la soka Ufaransa linafaa kujiuliza maswali mengi sana kwa kuangazia matokeo ya Ligi ya mataifa ya Ulaya. Didier Deschamps, anatakiwa kuwa makini amewapa Ufaransa ubingwa wa Kombe la Dunia ila kinachoendelea sasa sio soka la kiwango cha mabingwa wa dunia, anapaswa kutafuta mbinu mbadala la sivyo, Zinedine Zidane yupo na anahitaji sana nafasi hiyo.

Kocha wa Uigereza Gareth Southgate
Kocha wa Uigereza Gareth Southgate POOL/AFP

Gareth Southgate - Uingereza ni mojawapo ya mataifa ambayo yana wachezaji wazuri zaidi katika kizazi cha sasa. Sifa kubwa ya Uingereza pia ni kuwa wana ligi bora duniani. Ila sasa tatizo ni kocha mwenye kutumia wachezaji hao vizuri.

Tayari Uingereza imeshushwa daraja kwenye ligi ya mataifa ya ulaya baada ya kushindwa kuandikisha ushindi kwenye mechi sita kwa mara ya kwanza tangu Oktoba mwaka 1966 na kushindwa kufunga bao kwa mechi tatu kwa mara ya kwanza tangu Novemba mwaka 2000.

Mbinu za kocha kwenye uteuzi wa kikosi na nafasi anazochezesha wachezaji ndio chanzo. Kwa mfano; tuliona Kyle Walker  dhidi ya Italia akichezeshwa kama beki wa kushoto ilhali yeye ni wa kulia, kwa nini uwe na mabeki wanne wa kulia na wawili tu wa kushoto kikosini?

Bukayo Saka ambaye ni winga wa kulia kwa wakati fulani alionekana akicheza kama beki wa kupanda na kushuka ubavu wa kushoto ambapo kawaida Saka hucheza kama winga wa kulia wala si beki wa kupanda na kushuka. Ni wazi kuwa Gareth Southgate hatawapeleka Uingereza mbali na iwapo atasafiri nao hadi Qatar basi sidhani kama Uingereza watafika hatua ya kumi na sita bora.

Mtazame Fikayo Tomori, beki ambaye ameshinda taji la ligi kuu soka Italia msimu jana akiwa na AC Milan. Msimu huu amecheza mechi zote za ligi kuu Italia lakini hatapewa nafasi hata jana usiku dhidi ya Ujerumani hakujumuishwa kikosini.

Ila (beki Harry Maguire ambaye amecheza mechi tatu tu za Manchester United msimu huu na Conor Coady ambaye alikuwa nahodha wa Wolves akahamia Everton kwa mkopo kwa sababu ya kukosa kuonyesha fomu nzuri) wanapewa nafasi na kumuacha nje Fikayo Tomori. Ni suala la upendeleo kwenye uteuzi au?

Itokee labda Southgate ataipeleka Uingereza nchini Qatar basi kudumu kwake kama kocha kutategemea sana matokeo atayoandikisha kwenye kombe la dunia.  

Yote tisa kumi ni kwamba, uwezo wa kuwaajiri na kuwatimua makocha upo mikononi mwa shirikisho. Ila iwapo hao makocha watatu watasalia pale basi tuwe tayari kuona hayo mataifa wakiaga kombe la dunia mapema sana kinyume na matarajio ya hadhi na vikosi vilivyoshiba talanta.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.