Pata taarifa kuu
UCHAMBUZI

Uchambuzi: Kenya inahitaji Waziri wa Michezo mwenye sifa gani?

Uchaguzi umekamilika nchini Kenya, rais mpya ameapishwa  na tayari ameanza kazi rasmi. Ila bado wananchi nchini humo wanasubiri rais William Ruto kutaja baraza lake la mawaziri.

Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Naiorobi nchini Kenya
Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Naiorobi nchini Kenya pbs.twimg.com/medi
Matangazo ya kibiashara

Mashabiki wa michezo wana hamu kubwa kujua nani atarithi mikoba ya waziri anayeondoka Bi. Amina Mohammed. Waziri ni mkuu wa idara ya serikali.

Waziri wa michezo si mchezo wa soka, kwa sababu watu wengi hufikiri  michezo ni soka. La hasha ! Pia si wizara ya michezo tu bali ni wizara ya michezo, sanaa na utamaduni – kumaanisha kando na michezo, kuna utamaduni wa wakenya na sanaa ambayo waziri lazima ajukumike.

Kwa miaka mingi iliyopita nchini Kenya, serikali za hapo awali hazijakuwa zikiangazia sekta ya michezo kama sekta muhimu kwa hivyo kupewa mawaziri ambao hawafikishi michezo kwenye viwango vinavyofaa.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2021, waziri Hassan Wario alikumbwa na sakata la uvujaji wa fedha kwenye Olimpiki ya 2016 nchini Brazil. Kwa sasa, kila mchezo nchini humo unaonekana kudorora kutokana na kile mashabiki na wachambuzi wengi wanasema kuwa ni uongozi ambao hauelewi masuala nyeti kwenye sekta hiyo.

Shirikisho la kandanda limekumbwa na mgogoro dhidi ya wizara kwa miezi kumi na moja sasa, timu za taifa za voliboli, raga, magongo, basketboli, handboli, riadha pia zimekumbwa na changamoto ya usafiri na mishahara kwa wachezaji.  

Lisilo moyoni, na akilini pia halimo. Kitu cha kwanza, waziri huyu anastahili awe ni mpenzi wa michezo na sanaa. Awe ni mtu ambaye anaelewa kinachohitajika katika sekta hii muhimu kwa sababu wengi waliowekwa pale awali wanakosa ufahamu huo.

Mchambuzi wa michezo nchini Kenya, Greg Mulemi anasema, “Waziri awe ni mtu mwenye uwezo wa kufanya michezo iheshimike kwa kutumia sheria zilizowekwa kwenye mashirikisho tofauti. Pia awe ni mtu mwenye uwezo wa kuleta watu pamoja kwa sababu kuna mgawanyiko mkubwa sana wakati huu michezoni."

Ndio nitamuunga mkono kwa kuongeza kuwa sharti pia awe ni mtu mkweli, muadilifu, mwajibikaji na mwenye mbinu mwafaka kwenye usimamizi wa umma. Ila mashabiki wa michezo nchini Kenya wanamtaka waziri ambaye ana historia ya uanamichezo au amewahi kujihusisha pakubwa viwanjani.

Lakini mwanahabari mwenzangu studioni, Paul Nzioki anapinga hilo akisema kuwa waziri wa michezo nchini Tanzania Mohammed Omar Mchengerwa hajawahi kujihusisha viwanjani awali, alikuwa mbunge wa Rufiji hali sawa na waziri wa michezo nchini Uingereza Nigel Huddlestone.

Ni kweli si lazima awe na historia ya michezo, ila ufahamu na historia nzuri viwanjani, ni kigezo muhimu sana. Kwa mfano, mshindi wa kombe la dunia mara tatu na mfungaji bora wa timu ya taifa ya Brazil (kwa sasa, mabao 77), Pele alikuwa waziri wa kwanza wa michezo nchini humo kutoka 1995-1998.

Itakuwa afueni kubwa sana ikiwa atapatikana waziri ambaye ana vigezo hivyo vyote kwa pamoja kwani itaashiria mwamko mpya kwenye michezo nchini Kenya. Mamlaka anayo rais William Ruto.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.