Pata taarifa kuu
MASHINDANO YA JUMUIYA YA MADOLA 2022

Mashindano ya Jumuiya ya Madola Birmingham Uingereza

Mashindano ya Jumuiya ya Madola yameingia siku yake ya pili Birmingham Uingereza ambapo waafrika kutoka mataifa mbali mbali wanaendelea kujinyakulia medali.

Ferdinand Omanyala, anayeshiriki katika mashindano ya Jumuiya ya madola nchini Uingereza
Ferdinand Omanyala, anayeshiriki katika mashindano ya Jumuiya ya madola nchini Uingereza AFP - YASUYOSHI CHIBA
Matangazo ya kibiashara

Mbio za masafa marefu kwa upande wa kina dada na wanaume zimekamilika ambapo Mganda Victor Kiplagat na raia wa Australia Jessica Stenson wameshinda dhahabu kwa wanaume na wanawake mtawalia.

Kwa upande wa wanaume, Afrika Mashariki imetawala kwa kunyakua nafasi za tatu za kwanza. Victor Kiplagat alimaliza kwa muda wa saa 2:10:55 na kuwa raia wa Uganda wa kwanza kushinda dhahabu ya jumuiya ya madola.

Mtanzania Alphonce Simbu ambaye alishinda medali ya fedha katika mashindano ya dunia ya mwaka 2017 na kuwa wa tano na saba katika Makala mawili ya Olimpiki yaliyopita, alimaliza wa pili.

Mkenya Michael Githae ambaye alimaliza nafasi ya kumi kwenye Olimpiki ya mwaka jana, alishinda medali ya shaba kwenye mbio za leo jijini Birmigham.

Kwa upande wa kina dada, bingwa mtetezi Helalia Johanes mwenye miaka 41 kutoka Namibia alishindwa kutetea dhahabu yake aliyoshinda mwaka 2018 nchini Australia kwa kumaliza nafasi ya tatu. Mkenya Margaret Muriuki alishinda fedha huku Jessica Stenson akinyakua dhahabu.

Kwenye raga ya wachezaji saba kila upande, Kenya Shujaa 7s imefuzu hatua ya robo fainali ya mashindano baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi D. Shujaa imepoteza mechi yake ya mwisho 7-5 dhidi ya Australia leo asubuhi baada ya kuishinda Uganda 27-14 na Jamaica 45-0 jana. Afrika Kusini imefuzu robo fainali baada ya kuongoza kundi B.

Baadaye leo usiku, mkenya Nick Okoth atapambana na Keevin Allicock kwenye raundi ya 32 ya ndondi wakati pia timu ya Kenya ya voliboli ya ufukweni itachuana na New Zealand.

Hadi sasa, Australia inaongoza kwa jumla ya medali 18, Uganda ni ya saba kwa medali moja, Kenya ni ya tisa kwa medali mbili nayo, Tanzania ni ya 12 kwa medali moja na Namibia ni ya 14 kwa medali moja.

 

Na Jaysen Sagini

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.