Pata taarifa kuu
UCHAMBUZI-SOKA-AFRIKA

Uchambuzi: Vlabu barani Afrika vinawahitaji wachezaji wa kigeni?

Nairobi – Je, unafikiri ni wakati vilabu vya  soka barani Afrika kuhusisha pakubwa wachezaji wa kigeni ili kufanya vizuri zaidi katika ligi za nyumbani.

 Aliou Dieng (Kulia), mchezaji wa klabu ya  Ah Ahly, akipambana na Thapelo Morena  wa Mamelodi Sundowns
Aliou Dieng (Kulia), mchezaji wa klabu ya Ah Ahly, akipambana na Thapelo Morena wa Mamelodi Sundowns REUTERS - SIPHIWE SIBEKO
Matangazo ya kibiashara

Katika safari yangu ya kufuatilia soka ya Afrika nitatumia mifano kutoka mataifa mbali mbali kuchambua swala hili. Vilabu vinapoasisiwa huwa kila klabu ina malengo yake.

Mengine ni biashara, kukuza talanta, kushinda mataji  ila soka ya sasa imegeuzwa kuwa biashara tofauti na zamani ilivyokuwa ni wa kuburudisha. Dunia ya sasa imeifanya soka kuwa biashara kwa asilikia kubwa.

Ligi ya Ulaya  ilipopangwa kuanzishwa na rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez mwezi Aprili mwaka 2021, kila klabu ingepata euro milioni mia tatu na thelathini kwa mwaka.

Hii ikiwa ni mara tatu zaidi ya hela anazopata mshindi wa kombe la klabu bingwa barani ulaya. Hili lilisababishwa na vilabu kufanya usajili wa wachezaji ghali na wengi wa kigeni ili kufanikiwa kunyakua mataji ya ulaya.

Wachezaji wa klabu ya TP Mazembe nchini DRC
Wachezaji wa klabu ya TP Mazembe nchini DRC stringer / AFP

Turejee Afrika, ambapo asilimia kubwa ya vilabu vinatumia wachezaji wa nyumbani lakini dhana hiyo imeanza kubadilika hivi karibuni.

Sasa tumeanza kuona wachezaji kutoka DRC, Rwanda, Uganda, Tanzania wakicheza ligi kuu Kenya. Wengine hata kutoka Brazil wameshiriki ligi kuu bara Tanzania na Kenya.

Sababu ya kufanya usajili wa aina hiyo ni kuongeza nguvu na kuchanganya tajriba kwenye kikosi.

Dhana ya kuwa na wachezaji wa DR Congo pekee kwenye ligi inamaanisha wanashindana wenyewe kwa wenyewe na itakuwa vigumu kutabiri wapinzani barani Afrika kwa sababu hawajatangamana nao uwanjani.

Ligi za Kaskazini mwa Afrika zinatumia wachezaji wa nyumbani kwa asilimia tisini ikilinganishwa na za kusini na mashariki. Afrika Kusini ni baadhi ya ligi tajika Afrika ambayo ina wachezaji kutoka kila taifa.

Mamelodi Sundowns inaruhusiwa kuchezesha wachezaji watano wazawa wa nyumbani na wengine saba wa kigeni. Inapaswa ligi za Afrika zihusishe raia wa kigeni pakubwa hata kwenye viti vya ufundi, marefarii ili mchezo uwe wa kitaalam zaidi.

Wachezaji wa klabu ya Simba SC nchini Tanzania
Wachezaji wa klabu ya Simba SC nchini Tanzania © SimbaSCTanzania

Simba SC ya Tanzania ilifika hatua ya robo fainali kwenye kombe la klabu bingwa barani Afrika kwa mara ya kwanza msimu wa 2018/19 baada ya kuhusisha wachezaji kumi na wawili wa kigeni akiwemo Gerson Fraga Vieira (Brazil), Clatous Chama (Zambia), Haruna Niyonzima (Rwanda), Meddie Kagere na Emmanuel Okwi (Uganda), kocha Patrick Aussems (Ubelgiji).

Miaka miwili baadaye Wekundu wa Msimbazi walifanikiwa kufika tena hatua hiyo baada ya usajili wa Francis Kahata na Joash Onyango (Kenya), Larry Bwalya (Zambia), Taddeo Lwanga (Uganda), Luís Jose Miquissone (Msumbiji), Bernard Morrison (Ghana) na kocha mfaransa Didier Gomes da Rosa.

Gor Mahia ya Kenya pia ilifanikiwa kufika hatua ya juu zaidi katika historia yao kwenye mashindano ya kombe la mashirikisho Afrika mwaka 2019 walipofika robo fainali. Wachezaji kama vile Shafique Batambuze na Erisa Ssekisambu (Uganda), Gnamian Yikpe (Ghana), Francis Mustapha (Burundi) na kocha kutoka Uturuki Hassan Oktay waliisaidia Gor kufika hatua hiyo.

Wachezaji wa Gor Mahia mwaka 2019
Wachezaji wa Gor Mahia mwaka 2019 Yasuyoshi CHIBA / AFP

Muingereza Dylan Kerr atakumbukwa na mashabiki wa Gor Mahia kuwa kocha wa pekee kuifikisha Gor Mahia hatua ya makundi kombe la mashirikisho kwa mara ya kwanza.

Miaka kumi iliyopita Gor Mahia imekua ikiajiri makocha wa kigeni kama vile Zdravko Logarusic (Croatia), Bobby Williamson na Frank Nuttal (Scotland), Vaz Pinto, Steve Pollack, Jose Marcelo Ferreira kwa nia ya kufanya vizuri katika mashindano ya bara Afrika.

Kwa hivyo, kuhusisha wachezaji wa kigeni itaongeza mafanikio kwa timu katika mashindano ya bara na pia kwa timu ya taifa.

Ila kuwahusisha kwa asilimia kubwa kupita viwango itachangia kuua talanta za nyumbani. Sharti mashirikisho ya soka kwa mataifa mbali mbali yazingatie kutoegemea upande mmoja.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.