Pata taarifa kuu
KENYA-MICHEZO-SOKA

Dennis Oliech kuichezea Gor Mahia mechi yake ya kwanza siku ya Jumapili

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Kenya Dennis Oliech ambaye wiki hii alisajiliwa na klabu ya Gor Mahia, anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza siku ya Jumapili.

Klabu ya kenya ya Gor Mahia ambayo Dennis Oliech ataichezea mechi yake ya kwanza siku ya Jumapili Januri 6, 2019.
Klabu ya kenya ya Gor Mahia ambayo Dennis Oliech ataichezea mechi yake ya kwanza siku ya Jumapili Januri 6, 2019. gormahiafc.co.ke
Matangazo ya kibiashara

Gor Mahia itakuwa katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi kumenyana na Mathare United, klabu ambayo Oliech alianza kuichezea kabla ya kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Oliech mwenye umri wa miaka 33, alitia saini mkataba wa miaka miwili na anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo yenye mashabiki wengi nchini Kenya.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Ambrose Rachier amenukuliwa akisema anaamini kuwa, Oliech amekuja kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa zamani Meddie Kagere aliyehamia klabu ya Simba nchini Tanzania mwaka 2018.

Mshambuliaji huyo anakumbukwa sana baada ya kufunga bao muhimu mwaka 2003 dhidi ya Cape Verde jijini Nairobi na kuisaidia Kenya kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika mwaka 2004.

Mara ya mwisho Oliech kuichezea Kenya ilikuwa ni Septemba 6, mwaka 2015 dhidi ya Zambia katika mechi ya kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika mwaka 2017 na kulemewa mabao 2-1 katika uwanja wa Nyayo.

Amewahi kucheza soka nchini Ufaransa, Qatar na Dubai.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.