Pata taarifa kuu
EURO 2016

Ujerumani, Poland, Uhispania zasonga mbele, Uturuki kusubiri hatma yake

Michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya 2016, imeendelea kushika kasi nchini Ufaransa, huku baadhi ya timu zikifanya miujiza kwenye mechi zao za lala salama, na vinara kujikuta wakiangukia pua.

Wachezaji wa Ujerumani wakimpongeza, Mario Gomez jezi namba 23, aliyeifungia timu yake bao la ushindi dhidi ya Ireland Kaskazini, 21 Juni 2016.
Wachezaji wa Ujerumani wakimpongeza, Mario Gomez jezi namba 23, aliyeifungia timu yake bao la ushindi dhidi ya Ireland Kaskazini, 21 Juni 2016. REUTERS/John SibleyLivepic
Matangazo ya kibiashara

Hapo jana mechi za kundi C na D zilipigwa kwenye viwanja vinne tofauti, ambapo kwenye kundi C, Ukraine walikuwa wakicheza na Poland, Ireland Kaskazini wakiwa na kibarua dhidi ya Ujerumani, huku kwenye kundi D, Jamhuri ya Czech wakicheza na Uturuki, wakatik Croatia wao walikuwa wenyeji wa Uhispania.

Kwenye mechi ya awali kati ya Ukraine na Poland, ilishuhudiwa mchezo huo ukimalizika kwa timu ya taifa ya Poland kufanikiwa kuchomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0, ushindi ambao ulikuwa muhimu kwa Poland, ambayo inashika nafasi ya 2 kwenye kundi lake nyuma ya mabingwa wa dunia Ujerumani.

Mchezaji wa Ukraine, Artem Fedetskiy, akiinamisha kichwa chini baada ya mechi na timu yake kuondolewa rasmi kwenye michuano ya Ulaya
Mchezaji wa Ukraine, Artem Fedetskiy, akiinamisha kichwa chini baada ya mechi na timu yake kuondolewa rasmi kwenye michuano ya Ulaya REUTERS/Yves Herman

Ukraine walioingia uwanjani kwa lengo la angalau kupata ushindi kwenye mechi yake ya mwisho, ilijikuta ikimaliza hatua ya makundi ya michuano ya mwaka huu, bila ya kuwa na alama yoyote baada ya kupoteza mechi zake zote tatu.

Mchezaji wa Poland aliyeingia kipindi cha pili, Jakub Błaszczykowski, ndiye aliyekuwa shujaa kwa timu yake na pigo kwa timu ya taifa ya Ukraine ambayo ilijikuta jahazi lake likizama kwa kukubali kichapo cha bao 1-0.

Poland inamaliza nyuma ya Ujerumani yenye alama 7 sawa na Poland lakinik zinatofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa, ambapo sasa itacheza na Uswis kwenye hatua ya 16 bora siku ya Jumamosi.

Mashabiki wa Poland wakishangilia baada ya timu yao kufuzu hatua ya kumi na sita bora.
Mashabiki wa Poland wakishangilia baada ya timu yao kufuzu hatua ya kumi na sita bora. REUTERS/Jean-Paul Pelissier

Kwenye mchezo mwingine wa kundi C, Ireland Kaskazini wao walikuwa na kibarua dhidi ya mabingwa wa dunia, timu ya taifa ya Ujerumani, kwenye mchezo uliomalizika kwa Ujerumani kufanikiwa kuchomoza na ushindi wa bao 1-0.

Bao pekee la Ujerumani lilifungwa na mshambuliaji wake makini, Mario Gomez, ambaye katika mechi mbili mfululizo za timu hiyo alianzia benchi.

kwa ushindi huo, Ujerumani inamaliza kama kinara katika kundi lake kwa kuwa na alama 7, mbele ya Poland nayol yenye alama saba, lakini timu hizi sasa zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ujerumani sasa itacheza na mshindi wa tatu kutoka kwenye kundi A, B au F, kwenye hatua ya 16 bora, mechi ambayol itachezwa siku ya Jumapili.

Ireland ya Kaskazini, yenyewe pamoja na kupoteza mchezo wake dhidi ya Ujerumani, inafanikiwa kufika kwenye hatua ya mtoano baada ya kuwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi na timu yenye nidhamu, ikiwa ni kwa mujibu wa kanuni mpya zinazotumiwa na Uefa kupata timu nne zilizomaliza kwenye nafasi ya tatu zitakazoingia kwenye hatua ya 16 bora.

Mechi za kundi D pia nazo zilipigwa, ambapo mechi iliyokuwa ikitazamwa na mashabiki wengi wa soka, ni ile iliyoikutanisha timu ya taifa ya Croatia iliyokuwa na kibarua dhidi ya Uhispania, kwenye mchezo ambao ulimalizika kwa Croatia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kocha mkuu wa Croatia, Ante Čačić, amewapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya waliowahi kuwa mabingwa wa dunia na mabingwa wa kombe la Ulaya mara mbili, ambapo amedai kuwa ushindi huu umedhihirisha uimara wa kikosi chake na kwamba wanauwezo wa kucheza na yeyote yule watakaekutana ae kwenye hatua ya 16 bora.

Wachezaji wa timu ya Croatia wakishangilia baada ya mechi dhidi ya Uhispania
Wachezaji wa timu ya Croatia wakishangilia baada ya mechi dhidi ya Uhispania REUTERS/Michael Dalder Livepic

Mabao ya Croatia yalifungwa na Nikola Kalinic na Ivan Perisc aliyekuwa pia nyota wa mchezo huo, huku lile bao la Uhispania likifungwa na mshambuliaji wa Juventus, Alvaro Morata.

Kipigo kwa timu ya Uhispania kimeonekana kuwashangaza wengi kwa kuwa kwa karibu kipindi chote cha kwanza na dakika 20 za kipindi cha pili, ilionekana wazi kuwa Uhispania walikuwa wamemiliki mchezo na pengine Croatia wasingeweza kupata bao, lakini matokeo yakawa vinginevyo.

Mechi nyingine kwenye kundi D, ilizikutanisha timu ya taifa ya Jamhuri ya Czech iliyokuwa na kibarua dhidi ya timu ambayo ilikuwa haipewi nafasi ya kuibuka na ushindi, timu ya taifa ya Uturuki.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uturuki wakishangilia baada ya timu yao kupata bao dhidi ya Czech
Wachezaji wa timu ya taifa ya Uturuki wakishangilia baada ya timu yao kupata bao dhidi ya Czech REUTERS/Carl Recine

Kwenye mchezo ambao Uturuki iliingia uwanjani ikiwa haina alama yoyote kwenye kundi lake dhidi ya Czech iliyokuwa tayari na alama moja kwenye kundi lake, ilifanya kile ambacho kocha wake alikitarajia na sio kingine bali kuibuka na ushindi.

Uturuki walifanikiwa kuwafunga Czech kwa mabao 2-0, kwenye mchezo ambao nik dhahiri kikosi cha kocha, Fatih Terim, kiliingia uwanjani kikiwa na lengo moja tu, la kuhakikisha timu yake inapata ushindi kitu ambacho kimetokea.

Mabao ya Uturuki yalifungwa na Burak Yilmaz na Ozan Tufan, mabao ambayo yalitosha kabisa kuzamisha jahazi la Jamhuri ya Czech ambayo kwenye mchezo wa jana ilicheza chini ya kiwango.

Uhispania sasa itacheza na Italia kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora, mchezo utakaokumbusha fainali ya mwaka 2012, huku Uswis yenyewe ikitarajiwa kucheza na Poland.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania wakimpongeza Morata baada ya kuifungia timu yake goli
Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania wakimpongeza Morata baada ya kuifungia timu yake goli REUTERS/Regis Duvignau Livepic

Timu ambazo zimefuzu hadi sasa hatua ya 16 bora, ni pamoja na Ufaransa, Uswisi, Wales, Uingereza, Slovakia, Ujerumani, Poland, Ireland Kaskazini, Croatia, Uhispania, Italia na Hungary.

Timu ambazo zinasubiri kujua hatma yao na ambazo zimemaliza kwenye nafasi ya tatu ni pamoja na Uturuki yenye alama 3 ikiwa na mabao mawili ya kufunga na manne iliyofungwa, Albania yenye alama 3, ikiwa na bao moja la kufunga na mabao 3 ya kufungwa.

Timu ambazo zimeshaondolewa kwenye michuano ya mwaka huu ni, Romania, Urusi, Ukraine na Jamhiri ya Czech.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.