Pata taarifa kuu
QATAR-FIFA-KOMBE LA DUNIA

Fifa kuchunguza tuhuma za wajumbe wa kamati ya Qatar kutoa rushwa kupewa nafasi kuandaa fainali za mwaka 2022

Kamati ya maandalizi ya michuano ya kombe la dunia nchini Qatar mwaka 2022, inatarajiwa kukutana na afisa mkuu wa uchunguzi wa shirikisho la kabumbu duniani fifa, Michael Garcia kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za rushwa zinazoikabii kamati hiyo.

Rais wa FIFA, Sepp Blatter akionesha bahasha iliyoipa ushindi nchi ya Qatar kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2022
Rais wa FIFA, Sepp Blatter akionesha bahasha iliyoipa ushindi nchi ya Qatar kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2022 Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu kati ya wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Qatar na afisa wa fifa, Garcia, unafanyika kufuatia kuongezeka kwa shinikizo toka kwa wadau wa michuano hiyo wanaotaka nchi hiyo inyang'anywe uandaaji wa fainali za mwaka 2022.

Shinikizo hili limekuja baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa huenda nchi ya Qatar ilitoa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa fifa walioamua na kuipa nafasi nchi ya Qatar kuandaa fainali hizo.

Kwenye taarifa iliyochapishwa na gazeti moja la Marekani la The Sunday Times, imeandika kwa kirefu kuhusu tuhuma za wajumbe wa kamati ya maandilizi ya Qatar, kuhonga fedha kwa wajumbe ili waipigie kura nchi hiyo kuandaa fainali za mwaka 2022.

Kwenye tuhuma hizi yumo aliyekuwa rais wa shirikisho la soka barani Asia, Mohamed Bin Hamam ambaye wakati fulani alitupwa nje kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais wa shirikisho la kabumbu duniani fifa kwa tuhuma za rushwa.

Taarifa ya gazeti hilo imesema kuwa Bin Hamam pamoja na wajumbe wengine, walitoa kiasi cha dola milioni 5 kwa wajumbe wa shirikisho hilo ili kuipigia kura nchi ya Qatar kushinda nafasi ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2022.

Aliyekuwa rais wa shirikisho la soka la Asia, Mohammed Bin Hammam
Aliyekuwa rais wa shirikisho la soka la Asia, Mohammed Bin Hammam REUTERS/Sergei Karpukhin

Shirikisho la kabumbu duniani Fifa kupitia kwa rais wake, Sepp Baltter imekanusha wajumbe wake kupewa rushwa kuipigia kura Qatar, tuhuma ambazo sasa kwa taarifa hizi za siri zilizovuja huenda zikaliabisha shirikisho hili.

Makamu wa rais wa Fifa, Jim Boyce akinukuliwa na vyombo vya habari vya Uingereza, amesema kuwa yeye atakuwa tayari iwapo kura hiyo itaitishwa upya kuamua tena nchi ambayo itapewa nafasi ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2022 nchini Qatar.

Makamu wa rais Boyce amesisitiza kuwa atakuwa tayari kupiga kura upya iwapo tu tuhuma hizi za gazeti la Sunday Times zitathibitishwa.

Kamati ya maandalizi ya Qatar imekanusha kuhonga fedha wajumbe wake na kwamba ilizawadiwa nafasi ya kuandaa fainali hizo kwa haki zote na ndio maana wajumbe wake waliunga mkono.

Cheikh Tamim,akisalimiana na rais wa shirikisho la kabumbu duniani, Fifa, Sepp Blatter
Cheikh Tamim,akisalimiana na rais wa shirikisho la kabumbu duniani, Fifa, Sepp Blatter REUTERS/Fadi Al-Assaad

Toka nchi ya Qatar kupewa nafasi ya kuandaa fainali za mwaka 2022, imekuwa ikikosolewa kwa sehemu kubwa na wadau wa mpira wa miguu duniani kwa madai kuwa haikuwa na vigezo wa sifa za kuandaa fainali hizo.

Mbali na tuhuma za rushwa nchi hiyo pia inadaiwa kuwa hali ya hewa ambayo itashuhudiwa wakati wa fainali hizo, haitakuwa nzuri hasa kwa wachezaji kutokana na kipindi ambacho fainali hizo zitakuwa zikifanyika kitakuwa ni kipindi cha joto.

Nyuzi joto wakati wa fainali hizo inatarajiwa kufikia zaidi ya nyuzi joto 50.

Tayari mchunguzi wa Fifa, Garcia alishaanza uchunguzi rasmi kuhusu tuhuma za kutolewa kwa rushwa kwa nchi zilizopewa kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 na mwaka 2022.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.