Pata taarifa kuu
SOKA

Platini apendekeza timu 40 kushiriki kombe la dunia la mchezo wa soka kuanzia 2018

Rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya Michel Platini anapendekeza kuwe na timu 40 badala ya 32 katika mashindano yajayo ya kombe la dunia kuanzia mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

Platin anasema kuwa kuongezwa kwa timu nane zaidi katika michuano hiyo kutasaidia kuongeza timu zinazoshiriki katika fainali hizo hasa kutoka barani Afrika na Asia bila ya kupunguza zile kutoka barani Ulaya.

Bara la Ulaya hutoa timu 13 katika michuano hiyo huku, Afrika ikitoa timu tano sawa na bara la Asia ambalo wakati mwingine hutoa nne.

Ombi hili linakuja wiki moja tu baada ya rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter kusema kuwa mabara la Afrika na Asia yanahitaji uwakilishi zaidi kwa sababu wana uanachama mkubwa ikilinganishwa na bara la Ulaya na Marekani Kusini.

Platin ambaye ni mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Ufaransa anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Baltter baada ya kumaliza muda wake 2015, ameongeza kuwa ikiwa timu nane zaidi zitaongezeka basi michuano ya kombe la dunia itachezwa kwa siku tatu zaidi.

Rais huyo wa UEFA amesisitiza kuwa itakuwa vizuri ikiwa mabadiliko haya yataanza kushuhudiwa wakati wa kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018 ambapo timu mbili zaidi zitatoka barani Afrika na kufikisha idadi kuwa saba, mbili zaidi kutoka barani Asia na Marekani na moja zaidi kutoka barani Ulaya.

Kombe la kwanza la duniani la mchezo wa soka lilifanyika mwaka 1930 na wakati huo kulikuwa tu na timu 13, idadi ikaongezeka  hadi 16 mwaka 1934, kabla ya kuwa timu 24 mwaka wa 1982 na baadaye kuongezeka hadi 32 mwaka 1998.

Michuano ya mwaka 2014 ya kombe la dunia itafanyika nchini Brazil na bado michuano ya kufuzu inaendelea kote dunia kusaka mataifa 32 yatakayoshiriki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.