Pata taarifa kuu
KOMBE LA DUNIA 2014-BRAZIL

Mechi za soka za mzunguko wa mwisho kuelekea kombe la dunia kuchezwa mwishoni mwa wiki

Michuano ya soka ya mzunguko wa mwisho baina ya mataifa ya Afrika kutafuta nafasi ya kufuzu katika kombe la dunia nchini Brazil mwaka ujao inachezwa mwshoni mwa juma hili.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumamosi, Burkinafaso watakuwa nyumbani jijini Ouagadougou kumenyana na Algeria huku Cote Dvoire  pia wakiwa nyumbani jijini Abidjan kuchuana na Senegal.

Jumapili, Ethiopia watamenyana na Nigeria jijini Addis Ababa, Tunisia wacheze na Cameroon jijini Tunis  huku Ghana wakiwa nyumbani wachuane na Misri siku ya Jumanne juma lijalo mjini Kumasi.

Burkinafaso watakuwa uwanjani wakiwa na rekodi nzuri ya kumaliza wa pili katika michuano ya kuwania taji la mataifa ya Afrika mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Vijana wa Stallions wana dakika 180 nyumbani na ugenini kutinga kombe la dunia nchini Brazil na kocha Paul Put anasema mchuano wa Jumamosi utaamua mustakabali wa timu yake katika michuano hii kuwa miongoni mwa timu tano zitakazowakilisha bara la Afrika katika mashindano hayo.

Hata hivyo, Burkinafaso itamkosa mshambulizi wake wa kutegemewa Alain Traore ambaye alipata jeraha wakati wa michuano ya kombe la mataifa mwezi Januari na nafasi yake sasa itachukuliwa na Jonathan Pitriopa ambaye kocha Put anasema anaweza kufunga mabao wakati wowote.

Algeria ambayo imewahi kufuzu katika kombe la dunia mara tatu ikiongozwa na nahodha wao Madjid Bougherra amekiri kuwa Burkinafaso itakuwa timu ngumu kuishinda nyumbani kwao lakini wachezaji wenzake wamejiandaa vya kutosha kukabiliana na wapinzani wao.

Mchuano mwingine ambao pia utakuwa unaangaziwa Jumamosi hii ni kati ya Senegal na Cote Dvoire.

Washambulizi wa Cote Dvoire kama Didier Drogba na Solomon Kalou wanatarajiwa kuongoza mashambulizi kulisakama goli la Senegal katika mashambulizi ambayo yanatarajiwa kujibiwa na washambulizi wa Teranga Lions wakiongozwa na Papiss Cisse.

Mchuano wa marudiano utachezwa nchini Morroco baada ya shirikisho la soka duniani FIFA kuupiga marufuku uwanja wa Dakar kuandaa michuano ya kimataifa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mataifa matano ndio yatakazofuzu kuliwakilisha bara la Afrika katika michuano hiyo ya kombe la dunia nchini Brazil itakayofanyika mwezi Juni mwakani.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.