Pata taarifa kuu
SOKA-CHELSEA-UEFA

Mourinho aondoka kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari baada ya kuchukizwa na maswali ya Wanahabari

Kocha Mkuu wa Klabu ya Chelsea Jose Mourinho amechukizwa na maswali ya wanahabari kwenye Mkutano wake kabla ya kuchezwa kwa Mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest juu ya upangaji wake wa kikosi chake cha kwanza.

Kocha Mkuu wa Chelsea Jose Mourinho akiondoka kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari baada ya kuchukizwa na maswali
Kocha Mkuu wa Chelsea Jose Mourinho akiondoka kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari baada ya kuchukizwa na maswali
Matangazo ya kibiashara

Mourinho amekasirishwa mno na maswali yaliyokuwa yameelekezwa kwake kitu ambacho kilimkera na kumfanya aondoke kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari na kuwaambia wanahabari yeye ataendelea na msimamo wake.

Kocha huyo aliwaambia wanahabari amekuwa akimchagua mchezaji kuwepo kwenuye kikosi cha kwanza kutokana na uwezo anaouonesha kwenye mazoezi hivyo hafanyi kitu kwa kushinikizwa.

Mourinho alikasirishwa na swali la wanahabari waliokuwa wanataka kujua ni kwa nini amekuwa hawapi nafasi Kevin De Bruyne na Juan Mata ambapo mwenyewe alisema wachezaji hao wataanza kwenye mchezo wa leo.

Kocha huyo wa The Blues aliwaambia wanahabari ya kwamba anashangaa ni kwa nini amekuwa akiulizwa maswali kuhusiana na wachezaji wasiocheza pekee badala ya kujadili wachezaji wanaocheza.

Mourinho amesema amekuwa akiweka wachezaji nje ya kikosi cha kwanza kutokana na baadhi ya wachezaji kucheza chini ya viwango kwenye michezo iliyopita hasa ya Capital One dhidi ya Swindon.

Kocha huyo wa Chelsea amesisitiza uamuzi wa kumchagua mchezji kuwepo kwenye kikosi cha kwanza ni wake na hawezi kuchagua mchezaji kwa shinikizo lolote kutoka kwa wanahabari.

Mourinho amesema baada ya kuanza kumchagua Mata kwenye kikosi chake anashangaa wanahabari wameacha kumuuliza juu yake na badala yake wameelekeza nguvu zao kwa De Bruyne.

Kikosi cha Chelsea kinatarajiwa kushuka dimbani kukabiliana na Steaua Bucharest kwenye mchezo wa pili wa Kundi E ikiwa ni harakati za kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.