Pata taarifa kuu
UHISPANIA-LA LIGA

Real Madrid yasitisha sherehe za Ubingwa wa Barcelona baada ya kutoa kichapo kizito kwa Malaga

Real Madrid imesababisha Barcelona kwa mara nyingine kushindwa kusherehekea Ubingwa wa mapema katika La Liga baada ya hiyo jana kupata ushindi wa magoli 6-2 dhidi ya Malaga.

Wachezaji wa Real Madrid wakishangilia moja ya magoli waliyofunga dhidi ya Malaga
Wachezaji wa Real Madrid wakishangilia moja ya magoli waliyofunga dhidi ya Malaga
Matangazo ya kibiashara

Barcelona itaendelea kusubiri hadi mwishoni mwa juma watakapopata pointi moja ili waweze kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa La Liga wakiwavua ubingwa huo majasimu wao Real Madrid.

Real Madrid jana walifanikiwa kuvuna ushindi mnono wa magoli 6-2 dhidi ya Malaga iliyolazimika kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji tisa katika mchezo uliopigwa katika Dimba la Santiago Bernabeu.

Kocha Jose Mourinho alishusha kikosi chake kamili kwenye mchezo huo kasoro beki wa kati Pepe huku nahodha msaidizi Sergio Ramos akikosekana kutokana na kusumbuliwa na maumivu.

Real Madrid ilikuwa ya kwanza kupata goli la mapema kupitia beki wake Raul Albiol kabla ya Vijana wa Malaga hawajasawazisha kwa goli lililofungwa na Roque Santa Cruz kabla ya Cristiano Ronaldo hajakosa penalti Malaga wakiwa kumi baada ya Sergio Sanchez kulimwa kadi nyekundu.

Ronaldo alifunga goli la pili kwa Real Madrid kwa faulo na kufikisha goli la 200 tangu ajiunge na klabu hiyo kabla ya Mesut Ozil hajafunga goli la tatu na ndipo Malaga wakapata goli la pili lililofungwa na Vitorino Antunes.

Real Madrid ikaongeza kasi ya mashambulizi na hatimaye kujipatia magoli mengine matatu yaliyofungwa na Karim Benzema, Luka Modric na Angel Di Maria na kuwapa ushindi huo mzito wa nyumbani.

Barcelona watalazimika kuendelea kusubiri hadi mwishoni mwa juma watakaposhuka dimbani kupambana na Atletico Madrid siku ya jumapili na iwapo watashinda ni wazi watakuwa wametwaa taji hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.