Pata taarifa kuu
UEFA-UHISPANIA

Michezo miwili ya Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kupigwa nchini Uhispania

Michezo miwili ya mwisho ya mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya inatarajiwa kupigwa hii leo katika viwanja viwili tofauti ambapo Malaga FC watakuwa wenyeji wa Borussia Dortmund huku Real Madrid ikiwaalika Galatasaray. Michezo hiyo miwili ndiyo itatamatisha mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali iliyokuwa na michezo minne na tayari michezo miwili ilishuhudiwa ikipigwa jana nchini Ufaransa na kule Ujerumani.

Wachezaji wa Real Madrid na wale wa Galatasaray kabla ya mchezo wao wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya
Wachezaji wa Real Madrid na wale wa Galatasaray kabla ya mchezo wao wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya
Matangazo ya kibiashara

Malaga FC watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa La Rosaleda kuwaalika Borussia Dortmund ambao msimu huu wamekuwa na matokeo mazuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Kocha wa Malaga FC Manuel Pellegrini amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo muhimu na watautumia uwanja wao wa nyumbani ili kupata matokeo mazuri kabla ya marudiano yatakayofanyika juma lijalo.

Pellegrini amewataka wachezaji ake kucheza kwa umakini mkubwa na kutafuta goli la mapema ambalo linaweza likawasaidia kwenye harakati zao za kutinga hatua ya Nusu Fainali.

Naye Kocha wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp ameweka bayana wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo wakiamini ushindi wa ugenini utawasaidia kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Klopp anawategemea wachezaji wake Jakub Blaszczykowski, Mario Goetze, Marco Reus na Robert Lewandowski ambao anaamini watasaidia kwenye kiungo na upande wa ushambuliaji kuweza kupata magoli.

Mchezo mwingine utapigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu ambapo Real Madrid watakuwa wenyeji wa Galatasaray kuendelea na harakati zao za kuhakikisha wanatinga hatua ya Nusu Fainali.

Kocha wa Madrid Jose Mourinho amesema wapo tayari kwa mchezo huo huku akitarajiwa kuwatumia wachezaji wake mahiri akiwemo Cristiano Ronaldo na Xabi Alonzo kuweza kupata ushindi.

Mourinho ambaye amekataa kueleza hatima yake ya baadaye kama atasalia Santiago Bernabeu anaamini kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Barani ulaya ni miongoni mwa mafanikio anayoyaota.

Galatasaray inayonolewa na Fatih Terim nayo imejiandaa kukabiliana na Real Madrid kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote kutokana na uwezo wa wachezaji wa pande zote mbili.

Terim anatarajiwa kuwatumia Didier Drogba na Wesley Sneijder kwenye mchezo huo wa leo kutokana na wachezaji hao kufahamu fika mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa na Mourinho wakati akizinoa Chelsea na Inter Milan.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.