UEFA yasisitiza haihitaji teknolojia ya kubaini ikiwa mpira umevuka mstari
Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya Michel Platini amekariri msimamo wake wa hapo awali kuwa teknolojia mpya ya kubaini ikiwa mpira umevuka mstari au la usitumiwe katika mashindano ya UEFA.
Imechapishwa:
Majaribio ya teknolojia hiyo yameanza kutumiwa katika mashindano ya kutafuta bingwa wa klabu bora duniani yanayoendelea nchini Japan.
Platin ameongeza kuwa ni afadhali kuwatumia marefarii wanaosimama nyuma ya mlingoti ya magoli mfumo ambao UEFA imekuwa ikitumia kuanzia mwaka 2009 kubaini ikiwa mpira umevuka mstari au la.
UEFA inasema itaigharimu Euro Milioni 50 kuweka mitambo hiyo ya teknolojia ikilinganishwa na ikiwa wangeajiri marefarii ambao gharama itakuwa ya chini .
Teknolojia ya The Hawk-Eye itakuwa inatumia kati ya kamera sita na nane zitakazofungwa katika mlingoti ya magoli hayo huku ile nyingine ya GoalRef ikibaini ikiwa mpira utakuwa umevuka mstari.
FIFA inasema itatumia mfumo huo wakati wa mashindano ya kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014.