Pata taarifa kuu
UCHUMI-HAKI

Korea Kusini: Naibu kiongozi wa Samsung aachiliwa huru kwa msamaha wa rais

Bilionea anayetarajiwa kurithi kampuni ya Samsung Lee Jae-yong ameachiwa huru Ijumaa Agosti 12 baada ya kupewa msamaha wa rais. Huu ni mfano wa hivi punde wa mila ya Korea Kusini ya kuwasamehe wajasiriamali waliopatikana na hatia ya ufisadi na uhalifu mwingine wa kifedha.

Lee Jae-yong ni mtu wa 278 tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa shirika la Forbes, ambaye ameachiliwa huru kwa msamaha wa rais Agost 12, 2022.
Lee Jae-yong ni mtu wa 278 tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa shirika la Forbes, ambaye ameachiliwa huru kwa msamaha wa rais Agost 12, 2022. © Yonhap via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Bilionea Lee Jae-yong, aliyepatikana na hatia ya hongo na ubadhirifu mnamo mwezi wa Januari 2021, "ataruhusiwa kuendelea na kazi yake" ili "kusaidia kukabiliana na mzozo wa kiuchumi unaoikabili Korea Kusini," Waziri wa Sheria Han Dong-hoon amesema.

Lee Jae-yong ni mtu wa 278 tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa shirika la Forbes na aliachiliwa kwa dhamana Agosti 2021, baada ya kutumikia kifungo cha miezi 18 gerezani, zaidi ya nusu ya kifungo chake cha awali. Msamaha wa leo Ijumaa utamruhusu kurejea kazini kikamilifu, na kuondoa marufuku ya kuajiri ambayo aliwekewa na mahakama kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kifungo chake jela.

"Kutokana na msukosuko wa kiuchumi duniani, nguvu na uhai wa uchumi wa taifa umezorota, na kuna hofu kwamba mdororo wa uchumi utachukuwa kipindi kirefu," wizara ya sheria imesema katika taarifa yake. Wizara inatumai bilionea huyo anaweza "kuongoza chombo cha ukuaji uchumi nchini kwa kuwekeza kikamilifu katika teknolojia na kutoa ajira."

Wafanyabiashara wengine watatu wasamehewa

Lee Jae-yong amepewa msamaha huo pamoja na wafanyabiashara wengine watatu, akiwemo Mwenyekiti wa Kundi la Lotte, Shin Dong-bin, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela katika kesi ya ufisadi mwaka wa 2018. Ni naibu kiongozi wa Samsung Electronics, kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza simu mahiri duniani. Mapato ya jumla ya kampuni hiyo ni sawa na moja ya tano ya pato la taifa la Korea Kusini.

Alifungwa jela kwa makosa yanayohusiana na kashfa kubwa ya ufisadi iliyomwangusha rais wa zamani Park Geun-hye. Pia alikuwa amepatikana na hatia ya matumizi haramu ya propofol, dawa ya ganzi yenye nguvu. Ni jambo la kawaida kwa matajiri wakuu wa Korea Kusini kushutumiwa kwa ufisadi, ubadhirifu, ukwepaji kodi au shughuli nyingine haramu za kiuchumi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.