Balozi wa Marekani nchini Urusi kurudi Washington kwa Mashauriano
John Sullivan, balozi wa Marekani nchini Urusi, atarudi nchini Marekani wiki hii kwa mashauriano, kabla ya mkutano uliopangwa kati ya Marais Joe Biden na Vladimir Putin, shirika la habari la Ria limeripoti leo Jumanne.
Imechapishwa:
Wiki iliyopita Urusi iliwafukuza wanadiplomasia 10 wa Marekani kwa kulipiza kisasi Washington baada ya hatua yake ya kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, wakati huo alipendekeza John Sullivan kurudi Washington kwa mashauriano, kulingana na shirika la habari la Interfax.
Washington wiki iliyopita ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Urusi na kuweka vikwazo mbali mbali dhidi ya Urusi, ikiishtumu Moscow kwa kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani mwezi wa Novemba mwaka uliyopita, vitendo vya udukuzi wa kimtandao na uhasama dhidi ya Ukraine.