Zaidi ya watu 40 wauawa Nepal
Zaidi ya watu 40 wameuawa kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumanne wiki hii katika eneo la milimani nchini Nepal. Tetemeko hilo la ardhi limesababisha maporomoko ya ardhi na majengo kadhaa kuporomoka.
Imechapishwa:
Wakuu nchini Nepal sasa wamethibitisha kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na tetemeko jingine jipya lililotokea nchini humo, imepanda na kufikia zaidi ya watu 40.
Tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa kipimo cha Richter 7.3 limesababisha hasara kubwa katika wilaya za kaskazini mashariki ya mji mkuu Kathmandu na kuleta hofu katika taifa hilo ambalo tayari liko katika mshituko mkubwa na likijaribu kurejea katika hali ya kawaida.
Tetemeko hilo kubwa lililosikika hadi nchini India, lilisababisha vifo vya watu watatu huko. Mji wa Namche Bazaar, karibu na mlima Everest umeshuhudia maafa makubwa.
Aprili 25 kulishuhudiwa tetemeko kubwa nchini Nepal, ambapo watu 8,150 waliuawa na wengine wengi kuwaacha bila makaazi .
Taarifa zilichelewa kufika mji mkuu Kathmandu baada ya tetemeko la leo, lakini maafisa na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wamesema wanatarajia idadi ya vifo itapanda.
Madhara ya tetemeko hili hayajabainika ila inasemekana kuwa lilitikisa mji mkuu wa India New Delhi, vilevile mji mkuu wa Bangladesh Dhaka.