Pata taarifa kuu

Miili ya wanajeshi wa Marekani waliouawa Jordan kurejeshwa nyumbani

Nairobi – Miili ya wanajeshi watatu wa Marekani waliouawa katika kambi ya jeshi huko Jordan, inatarajiwa kuwasili nchini humo leo Ijumaa.

Rais Biden amesema nchi yake itajibu shambulio hilo dhidi ya maofisa
Rais Biden amesema nchi yake itajibu shambulio hilo dhidi ya maofisa © Reuters
Matangazo ya kibiashara

Rais Joe Biden anatarajiwa kupokea miili ya maofisa wa nchi yake walioauwa katika shambulio la ndege isio na rubani, shambulio ambalo Washington inasema lilitekelezwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran.

Hawa ni maofisa wa kwanza wa jeshi la Marekani kuuawa mashariki ya kati tangu kuanza kwa mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas tarehe 7 ya mwezi Oktoba mwaka wa 2023.

Makabiliano yamekuwa yakiripotiwa kati ya vikosi vya Marekani na waasi wanaodaiwa kuungwa mkono na nchi ya Iran nchini Iraq na Syria pamoja na wapiganaji wa Huthi nchini Yemen.

Miili ya wanajeshi hao William Jerome Rivers, Kennedy Ladon Sanders na Breonna Alexsondria Moffett inatarajiwa kuwasili katika uwanja wa kijeshi wa Dover, huko Delaware, ambapo itapokelewa kwa heshima za kijeshi.

Rais Biden pia alipokea miili ya wanajeshi wengine waliouawa jijini Kabuli tarehe 26 mwezi Agosti mwaka wa 2021, maofisa waliouawa wakati Marekani ikiondoa vikosi vyake nchini Afghanistan.

Ikulu ya White House inasema wapiganaji waasi wa Islamic Resistance nchini Iraq ndio waliotekeleza shambulio dhidi ya maofisa hao nchini Jordan, karibu na mpaka na Syria.

Rais Biden bila ya kuweka wazi tarehe, ameapa kuwa nchi yake itajibu shambulio hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.