Pata taarifa kuu

Wakimbizi nchini Chad, Wasudan wanasimulia hali ya kutisha ya Darfur

Mzozo unaoendelea nchini Sudan umesababisha maelfu ya watu kukimbilia uhamishoni, hususan kukimbia ghasia huko Darfur ambako jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi kuhusu mauaji ya kikabila, na wengi wanapata hifadhi katika kambi zilizojaa watu katika jangwa la mashariki mwa Chad.

Wanawake wa Sudan wanapokea matibabu katika hospitali ya huko Adré, Chad, kwenye mpaka na Sudan.
Wanawake wa Sudan wanapokea matibabu katika hospitali ya huko Adré, Chad, kwenye mpaka na Sudan. © Mohaned Belal / AFP
Matangazo ya kibiashara

Akiwa ameketi chini, mbele ya makazi yake ya muda katika kambi ya Adré, mashariki mwa Chad, Mariam Adam Yaya, 34, anajaribu kutuliza njaa yake kwa kupasha moto chai kwenye kuni. Mwanamke huyo kutoka kabila lisilo la Kiarabu la Massalit, alivuka mpaka kwa miguu baada ya safari ya siku nne, bila chakula chochote, akiwa mtoto wake wa miaka minane mgongoni. Anadai kuwa alilazimika kuwatelekeza watoto wake wengine saba baada ya kushambuliwa kijijini kwake na wanaume "wenye silaha nzito".

Tangu Aprili 15, Sudan iinakumbwa na vita kati ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhane, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (FSR, wanamgambo) wanaoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdane Daglo.

Huko Darfur, raia ni wahanga wa ghasia kubwa ambazo zimeufanya Umoja wa Mataifa kuhofia mauaji mapya ya kimbari katika eneo hilo. "Tuliyopitia Ardamata ni ya kutisha. Vikosi vya usaidizi wa haraka, RSF, viliwaua wazee na watoto kiholela," ameliiambia shirika la habari la AFP.

Katika mji wa Ardamata pekee, huko Darfur Magharibi, zaidi ya watu 1,000 waliuawa mapema mwezi Novemba na makundi yenye silaha, kulingana na Umoja wa Ulaya. Ghasia hizi ziliwalazimu zaidi ya watu 8,000 kukimbilia nchi jirani ya Chad katika wiki moja, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Miji mikuu kadhaa ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Washington, imeshutumu "wanachama wa RSF na wanamgambo washirika kwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu na vitendo vya utakaso wa kikabila." Umoja wa Ulaya, "umefadhaika", pia unashuku "uangamizaji wa kikabila" huko Darfur.

Wakimbizi, mara baada ya kuwasili katika jimbo la mpakani la Ouaddaï, wanakusanyika katika kambi zinazosimamiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na katika nyingine zisizo rasmi, ambapo kuna makazi ya muda. Chad, taifa la Afrika ya kati ambalo ni la pili kwa maendeleo duni duniani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, lina idadi kubwa ya wakimbizi wa Sudan, ikiwa na watu 484,626 tangu kuanza kwa vita mwezi Aprili, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR).

Tangu kuwasili kwake nchini Chad, Mariam Adam Yaya na mtoto wake "hula mara chache", anaelezea shirika la habari la AFP. Ukosefu wa maji pia ni chanzo cha mvutano katika kambi, ambayo mashirika ya kibinadamu yaliyopo yanajitahidi kupunguza mvutano huo.

"Tuliwekwa chini katika makundi ya watu 20"

Akiwa ameketi juu ya kitanda katika jengo la matibabu ya dharura la shirika lisilo la kiserikali la Médecins Sans Frontières (MSF), lililo nje kidogo ya kambi ya Adré, Amira Khamis, mwanamke wa miaka 46 wa Massalit, anapumzisha miguu yake miwili iliyokatwa na bomu. Akiwa na kiwewe, mwathiriwa huyo, ambaye alipoteza watoto wake watano, anashuhudia unyanyasaji aliopata kwa sababu ya "kabila anakotoka". "Waliwaua watu wote wenye ngozi nyeusi," ameliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa alishuhudia ubakaji wa wanawake na wasichana wadogo.

Huku mkono wake wa kulia uliovunjika kusaidiwa na bandeji shingoni mwake, Mahamat Nouredine, kijana mwenye umri wa miaka 19, anathibitisha kamata kamata ya watu ya FSR dhidi ya watu kutoka jamii ya Massalit. "Kundi la FSR lilitufuata hadi hospitalini na kujaribu kuua kila mtu (...) walituweka chini katika makundi ya watu 20, na kutupiga risasi," anasema kijana ambaye alifanikiwa kukimbilia Chad. "Lengo lao ni kuua watu kwa sababu ya rangi ya ngozi zao," amebaini, akiomboleza mauaji ya watu wanne wa familia yake.

Mratibu wa mpango wa MSF huko Adré, Gérard Uparpiu, anasema "hali inazidi kuwa ya wasiwasi kutokana na wimbi la wakimbizi wapya wa Sudan." "Tunapokea watu hawa wanaofika wakiwa katika hali mbaya sana. Wamechanganyikiwa kimwili na kisaikolojia," ameongeza.

Hasa kwa kuwa safari ya kwenda Chad ilikuwa hatari kwa wakimbizi. "Pia walitushambulia nilipokuwa nikisafirishwa kwenda Chad kwa matibabu," anasema Amir Adam Haroun, mkimbizi wa Massalit ambaye mguu wake ulikatwa na vilipuzi.

Vita vya miezi minane vya Sudan vimesababisha vifo vya watu 12,000, kulingana na makadirio kutoka kwa shirika la Armed Conflict and Event Data Project, wakati Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 6.8 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.