Pata taarifa kuu

Iwobi: Nigeria itarejea katika ubora wake

NAIROBI – Kiungo wa kati wa timu ya taifa ya Nigeria, Alex Iwobi anawaahidi mashabiki wa Super Eagles kuwa kikosi hicho, kitarejea katika ubora wake, licha ya kufungwa bao 1-0 na Guinea Bissau siku ya Ijumaa, katika mchuano wa kufuzu kucheza fainali ya Afrika mwaka ujao nchini Cote D’ voire. 

Alex Iwobi mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria.
Alex Iwobi mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria. POOL/AFP
Matangazo ya kibiashara

Nigeria ambao wanajivunia mshambulizi shupavu kutoka klabu ya Napoli ya Italia, Victor Osimhen walipigiwa upato mkubwa kushinda mechi hiyo, lakini mambo yalikuwa tofauti, baada ya  Mala Balde kuipa Guinea Bissau bao hilo la ushindi. 

Iwobi ambaye anaichezea klabu ya Everton nchini Uingereza, amesema wachezaji wenzake wamekubali aibu na sasa wanaangazia michuano inayofuata. 

"Sisi kama timu ni lazima tuzinduke na kile ambacho tutafanya ni kujiboresha. Kwa mashabiki nitawaomba wasife moyo waendelee kutushangilia kwa sababu tunajitolea kwa hali na mali si kwa ajili yetu binafsi bali kwa taifa kwa ujumla," amesema Iwobi.  

Kufuatia ushindi wa Guinea Bissau sasa inashikilia uongozi wa kundi A kwa alama saba, Nigeria ni ya pili kwa alama sita, Sierra Leone ya tatu kwa alama mbili na Sao Tome Principe ni ya mwisho wakiwa na alama moja.   

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanasoka waliobobea walifanikiwa kufungia timu zao za taifa akiwemo Sadio Mane, Mohammed Salah na Sebastian Haller. 

Sadio Mane ambaye alirejea kwenye kikosi cha Senegal baada ya kukosa kombe la dunia kufuatia jeraha, alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mozambique jijini Dakar.   

Mo Salah alifunga bao la kwanza na kusaidia kupatikana kwa bao la pili katika ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Malawi jijini Cairo na kusonga kutoka nafasi ya mwisho hadi ya kwanza kwenye kundi D.   

Haller ambaye alirejea uwanjani mwezi jana baada ya kupokea matibabu ya saratani ya tezi dume, alifunga bao la pili la Ivory Coast katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Comoros mjini Bouake.   

Tanzania ilifanikiwa kupata ushindi wa goli 1-0 ugenini dhidi ya majirani wao Uganda. Bao hilo lilifungwa na Simon Msuva kipindi cha pili.    

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.