Pata taarifa kuu
MAANDAMANO-HAKI

Upinzani nchini Guinea walaani ukandamizaji mbaya wa maandamano

Maandamano ya Alhamisi nchini Guinea dhidi ya utawala wa kijeshi yalisababisha vifo vya raia watatu na kuwaacha takriban 20 wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi, kundi la waandalizi lilisema usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa, ripoti iliyopingwa na mamlaka.

Maandamano mjini Conakry tarehe 28 Julai, 2022. Utawala wa kijeshi wa Guinea umepiga marufuku maandamano tangu mwezi Mei 2022.
Maandamano mjini Conakry tarehe 28 Julai, 2022. Utawala wa kijeshi wa Guinea umepiga marufuku maandamano tangu mwezi Mei 2022. AFP - CELLOU BINANI
Matangazo ya kibiashara

Mwanasheria Mkuu wa Conakry Yamoussa Conté aliripoti, kwa upande wake, sita waliojeruhiwa katika safu ya vikosi vya usalama, ikiwa ni pamoja na watano wakiwa katika hali mbaya, na watu wawili kujeruhiwa miongoni mwa raia. Ameagiza kufunguliwa mashtaka "dhidi ya waandaaji na washiriki wote (katika) maandamano yaliyopigwa marufuku", katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyosomwa kwenye runinga ya serikali. Aliwataja hasa viongozi saba wa upinzani ambao wanadaiwa kuitisha maandamano au kuunga mkono mwito huo.

Vuguvugu la kiraia la FNDC lilitoa wito wa maandamano siku ya Alhamisi huko Conakry kudai kurejea haraka kwa raia madarakani na kuachiliwa kwa wafungwa wote wanaozuiliwa kwa sababu za kisiasa. Maandamano hayo yalizua mapigano kati ya vijana na vikosi vya usalama katika vitongoji kadhaa katika viunga vya mji wa Conakry.

Guinea imekuwa ikitawaliwa na serikali ya kijeshi inayoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya tangu kiongozi huyo na wanajeshi wake walipopindua mamlaka ya kiraia mnamo mwezi wa Septemba 2021. Jeshi hilo lilipiga marufuku maandamano na kutangaza kuvunjwa kwa vuguvugu la kiraia la FNDC.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa usiku kuamkia siku ya Ijumaa, FNDC ilielezea mamlaka ya sasa kama ya "kidikteta". Iliwataja raia watatu waliouawa ambao ni Thierno Bella Diallo, El hadj Boubacar Diallo na Thierno Moussa Barry. Pia imedai kwamba "watu wengi walikamatwa".

'Adhabu kali zaidi'

Vuguvugu la kiraia la FNDC limekuwa nyuma ya maandamano ya Julai 28 na 29, Agosti 17, na Septemba 5 na 6. Watu watano waliuawa mwezi Julai, na wawili mwezi Agosti. Limetoa wito tena kuandamana Oktoba 26 kote nchini.

Serikali ya kijeshi imeahidi kurudisha mamlaka kwa raia baada ya uchaguzi katika kipindi cha miaka mitatu. Serikali hiyo inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo inadai kipindi kifupi cha mpito.

Maandamano ya Alhamisi yalikuja wakati ujumbe wa ECOWAS ulikuwa ziarani nchini Guinea wiki hii kupanga ratiba kama hiyo na mamlaka.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.