Pata taarifa kuu

Mali: jeshi na wasaidizi wake watuhumiwa kwa ubakaji na uporaji Nia-Ouro

Nchini Mali, shutuma mpya za unyanyasaji zinalenga jeshi la Mali na wasaidizi wake kutoka Urusi - mamluki wa kundi la Wagner, ambao nchi nyingi za Magharibi na Afrika zinabaini kwamba, ni wakufunzi wa kawaida waliotumwa na serikali ya Urusi, kusaidia Bamako. 

Vikosi vya Wanajeshi wa Mali (FAMA) na wasaidizi wao kutoka Urusi wanatuhumiwa kwa ubakaji na uporaji katika kijiji cha Nia-Ouro katikati mwa nchi.
Vikosi vya Wanajeshi wa Mali (FAMA) na wasaidizi wao kutoka Urusi wanatuhumiwa kwa ubakaji na uporaji katika kijiji cha Nia-Ouro katikati mwa nchi. © AFP - MICHELE CATTANI
Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Mali na wasaidizi wake kutoka Urusi wanakabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kingono na ubakaji, ambazo zinadaiwa kufanywa Jumapili Septemba 4, 2022 katika wilaya ya Fakala, karibu na Sofara, eneo la Mopti, katikati mwa Mali, kulingana na vyanzo vingi vya ndani. 

Waliingia kijijini Tandiama kwa mara ya kwanza saa kumi na moja alfajiri. Wanajeshi wa Mali, wakiandamana na wasaidizi wao kutoka Urusi na wawindaji wa jadi wa Dozo, hawakufanya vurugu yoyote. Lakini katika kutafuta taarifa juu ya makundi ya kijihadi yanayoendesha harakati zao katika eneo hilo, waliwakamata wenyeji wawili, watu mashuhuri wa kijiji hicho.

Kisha, walielekea katika kijiji jirani cha Nia-Ouro. Kijiji ambacho tayari kimekuwa kikilengwa na dhuluma mbaya za jeshi mnamo mwezi wa Januari, madai ambayo yalikanushwa na mkuu wa jeshi ambaye walieleza kwamba walifanya "operesheni za kupambana na ugaidi". Lakini siku ya Jumapili, wakiwa wametahadharishwa kuhusu kuwasili kwa msafara wa wanajeshi na kuhisi kutishwa, wakazi wa kijiji hiki walikimbia kujificha msituni.

Picha na ubakaji

Wakati jeshi la Mali (FAMA) na washirika wake waliwasil katika kijiji hiki, walikuta wazee, walemavu ... na wanawake. Kulingana na taarifa zilizokusanywa kutoka kwa vyanzo vingi katika eneo hilo, wawindaji wa Dozo walipiga kambi katika kituo cha afyahuku askari wa Mali na wasaidizi wao wa Kirusi wakipiga kambi katika shule kijijini hapo.

Kisha wanawake waliamriwa kwenda nyumbani. Inasemekana mamluki kutoka kundi la Wagner ambao wakati wakikagua nyumba hizo waliwaamuru wanawake hao kuvua nguo. Waliwapiga picha kabla, wakati mwingine, kuwapapasa. Vyanzo kadhaa vinazungumza wazi juu ya ubakaji.

Uporaji mkubwa

Unyanyasaji huu wa kijinsia unaambatana na visa vya uporaji: vito, dhahabu, fedha, samani ... mifugo pia iliibiwa na wakazi kukamatwa. Wakazi wengi waliondoka kwenda kuomba hifadhi katika maeneo jirani ya Sofara - ambapo karibu yake kulikuwepo na kambi ya vikosi maalum vya Mali - na Tandiama.

Lilipoulizwa na RFI, jeshi la Mali halikutaka kujibu. Jumanne hii, wanajeshi na wawindaji wa dozo walikuwa bado wakiripotiwa kijijini.

Si mara ya kwanza jeshi la mali na wasaidizi wake kutoka Urusi kushtumiwa kwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono. Itakumbukwa wakati wa operesheni kubwa ya jeshi la Mali na wasaidizi wake dhidi ya magaidi huko Moura, mwezi Machi, jeshi la Mali na wasaidizi wake walishtumiwa kwa mauaji, uporaji na ubakaji.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.