Pata taarifa kuu
MCHEZO-TENNIS

Australia yasitisha kwa mara nyingine Visa ya Novak Djokovic

Nchi ya Australia, kwa mara ya pili imesitisha kibali cha kuingia nchini humo cha mchezaji maarufu wa tenesi, Novak Djokovic, kutokana na utata kuhusu haki ya kuendelea kubaki nchini humo bila ya kuwa amechoma chanjo dhidi ya UVIKO 19.

Novak Djokovic kutoka Serbia, ni bingwa wa mchezo wa Tennis duniani, Melbourne, Australia, Januari 13, 2022.
Novak Djokovic kutoka Serbia, ni bingwa wa mchezo wa Tennis duniani, Melbourne, Australia, Januari 13, 2022. AFP - MIKE FREY
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu uliotangazwa na waziri wa masuala ya uhamiaji wa Australia, Alex Hawke, amesema umechukuliwa kwa kuzingatia sheria ya afya ya taifa hilo, hatua inayomaanisha kuwa ana uwezo wa kumfukuza nchini humo.

Hata hivyo licha ya uamuzi huu, Djokovic, raia wa Serbia bado ana uwezo wa kufungua jalada jingine la kesi kipinga kufukuzwa nchini humo.

Djokovic ambaye anashikilia nafasi ya kwanza kwa ubora wa mchezo huo duniani, alikuwa amepangiwa kuanza lkucheza mechi yake ya kwanza ya mashindano ya Australian Open, yanayotarajiwa kuanza Jumatatu ya wiki ijayo.

Leo hii nimetumia mamlaka yangu, kusitisha hati ya kuwa nchini ya ndugu Novak Djokovic, kwa kuzingatia sheria ya amri ya afya, na ni kwa misingi ya afya ya uma pia. Ilisema taarifa ya waziri Alex.

Uamuzi huu una maana pia, huenda Djokovi akakabiliwa na adhabu ya kutoruhusiwa kupewa hati ya kuingia kwenye taifa hilo kwa muda wa miaka mitatu, licha ya kuwa adhabu hii inaweza kuondolewa.

Mshindi huyu mara 9 wa taji la Australian Open, alikuwa anatarajia kutetea taji hilo kuanzia wiki ijayo, ambapo ikiwa angeshinda, kungemfanya awe mchezaji tenesi wa kwanza mwanaume katika historia kushinda mataji makubwa 21 (Grand Slams).

Kwa mara ya kwanza hati yake ya kuwa nchini humo (Visa) ilibatilishwa saa chache tyu baada ya kuwasili kwenye mji wa Melbourne, Januari 6, baada ya mamlaka ya usimamizi wa mipaka kudai kuwa alishindwa kutoa uthibitisho unaohitajika ili kuonesha aliruhusiwa kitabibu kutokuchoma chanjo dhidi ya UVIKO 19.

Tangu igundulike kuwa mchezaji huyo hakuwa amechoma chanjo lakini akaruhusiwa kuingia nchini humo, kuliibua mjadala mkali miongoni mwa raia wa Australia.

Alizuiliwa kwa saa kadhaa katika uwanja wa ndege wa Melbourne na kisha baadae kutumia siku kadhaa akizuiliwa katika kituo maalumu cha wahamiaji, ambapo siku chache baadae hati yake ya kuwa nchini humo ilirejeshwa na jaji aliyeagiza mchezaji huyo kuachiwa kwa kile alichosema maofisa wa uhaliaji hawakufuata taratibu vizuri wakati alipowasili.

Hata hivyo licha ya kuwa alishaanza kufanya mazoezi peke yake, waziri wa masuala ya uhamiaji, Ijumaa hii akatangaza kusitisha hati (visa) ya mchezaji huyo kwa sheria tofauti ya uhamiaji.

Sheria hiyo inasema waziri anayo mamlaka ya kusitisha hati ya mtu yeyote ambaye ataonekana kuwa ni hatari kwa afya ya uma, usalama au tabia njema.

Hili linajiri wakati ambapo ni juma hili tu ambapo Djokovic alizungumzia madai ya kuwa alitoa taarifa za uongo wakati akijaza nyaraka zake za kusafiria, ambapo alidai hakuwa amesafiri katika muda wa siku 14 kabla ya kuwasili nchini Australia, wakati ukweli ni kwamba alisafiri kwenda nchini Hispania.

Mchezaji huyu pia alikiri wakati akihojiwa na mwandishi mmoja wa habari wa Ufaransa, kuwa alikuwa amethibitishwa kuambukizwa UVIKO 19 wakati alipoenda kupiga picha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.