Pata taarifa kuu

Ethiopia: Abiy asifu uchaguzi wa kihistoria, apata ushindi mkubwa

Chama tawala nchini Ethiopia, kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa wabunge uliofanyika mwezi uliopita, ushindi ambao unampa nafasi waziri mkuu Abiy Ahmed, kuongoza taifa hilo kwa kipindi kingine cha miaka 5 licha ya vita kwenye eneo la Tigray.

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Amanuel Sileshi AFP
Matangazo ya kibiashara

Waziri mkuu Ahmed, ameuelezea uchaguzi huo kuwa wa kihistoria, ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kupigiwa kura tangu alipochaguliwa kuwa waziri mkuu mpya wa taifa hilo mwaka 2018.

Abiy Ahmed, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019, alikuwa anatumia uchaguzi huu kujitengenezea njia ya kupata uungwaji mkono katika harakati zake za mabadiliko na operesheni za kijeshi kwenye eneo la Tigray.

Uchaguzi huu ambao ulikuwa tofauti na zile zilizopita kutokana na mazingira yanayoikabili nchi hiyo kwa sasa ikiwemo, vita kwenye eneo la Tigray na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19.

Chama chake kimeshinda viti 410 kati ya viti 436, matokeo haya ni kwa mujibu wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo.

Licha ya waziri mkuu Abiy Ahmed kusifia uchaguzi huu, waangalizi wa kimataifa waliokuwa nchini humo, wanasema licha ya kuwa ulifanyika kwa amani, haukuwa huru na wa haki.

Uchaguzi kuahirishwa mara mbili

Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huu, tume ya uchaguzi iliuahirisha mara mbili, mara ya kwanza kwa sababu ya ugonjwa wa Covid 19, na mara ya pili kutokana na kile tume ya uchaguzi ilisema haikuwa imejiandaa kufanya uchaguzi huo.

Hata hivyo licha ya uchaguzi huu kufanyika, maeneo mengi ya nchi katika jumla ya majimbo ya uchaguzi 547, hawakushiriki kwasababu mbalimbali ikiwemo miundombinu na machafuko.

Tume ya uchaguzi nchini humo hata hivyo haijasema ni lini uchaguzi kwenye eneo la Tigray, utafanyika wakati huu Serikali ikiwa imetangaza kusitisha mapigano huku wapiganaji wa eneo hilo wakitangaza kurejea kwenye mji mkuu wa jimbo hilo wa Mekele baada ya vikosi vya Serikali kuondoka.

Wachambuzi wa mambo wanaonya kuhusu uwezekano wa kushuhudiwa mapigano mapya kwenye eneo hilo hasa ikiwa Serikali itatangaza kumalizika kwa muda wa usitishaji mapigano.

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, juma hili limesema lilituma msafara wa magari ya chakula karibu 50 kwenye eneo la Tigray, lakini hadi sasa halijapata uthibitisho ikiwa chakula hicho cha msaada kilifika kutokana na kukatwa kwa mawasiliano kwenye eneo hilo.

Madai ya uchaguzi kuwa na dosari

Hata hivyo wakati tume ikitangaza matokeo, vuguvugu la upinzani la Amhara, limewasilisha malalamiko yake kwa tume ya uchaguzi, ukilalamika kuhusu kuwepo kwa dosari za msingi kwenye uchaguzi uliopita.

Vuguvugu hilo linasema waangalizi wake wengi wa uchaguzi walizuiwa kufika kwenye baadhi ya vituo vya kupiga kura ambapo baadhi walikamatwa, alisema afisa wa juu wa vuguvugu hilo, Dessalegn Chanie.

Baadhi ya taasisi za kimataifa zilizofuatilia uchaguzi wa Ethiopia, zinasema kwa sehemu kubwa vijana hawakushirikishwa kikamilifu katika siasa za nchi hiyo, ambapo zimeongeza kuwa kuna haja ya vijana kushirikishwa zaidi katika ngazi za maamuzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.