Serikali ya Algeria yatangaza maombolezo ya kitaifa ya siku tatu
Watu 257 walipoteza maisha siku ya Jumatano (Aprili 11) katika ajali ya ndege ya kijeshi ya Algeria karibu na uwanja wa ndege wa Boufarik, kilomita thelathini kusini mwa mji wa Algiers. Serikali ya Algeria imetangaza maombolezo ya kitaifa ya siku tatu. Algeria imekumbwa na mkasa mbaya kufuatia ajali hii.
Imechapishwa:
Ndege hii ya kijeshi Ilyushin II-76 ilianguka dakika tatu au nne baada ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufarik.
Rais Abdelaziz Bouteflika ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia siku ya Jumatano. Pia "ameagiza" kusaliwa siku ya Ijumaa Sala ya jeneza kwa waathirika, baada ya sala tukufu ya Ijumaa.
Ndege hiyo ya kijeshi ya usafiri ilianguka mara tu baada ya kuondoka kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufarik.
Ndege hii Ilyushin II-76 ilianguka katika shamba moja karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufarik. Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni askari na familia zao. Abiria 247 na wafanyakazi kumi wa ndege hiyo wote wameangamia katika ajali hiyo.
Ndege hiyo ilianguka katika "sehemu ya kilimo" muda mfupi baada ya kuondoka katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Boufarik huko Blida, kusini mwa Algiers.
Ndege hiyo ilikua ikielekea uwanja wa ndege wa kijeshi wa Tindouf, kwenye mpaka na Sahara Magharibi. Vyanzo vya Usalama, vilivyonukuliwa na gazeti la kila siku la Ennahar, vinabaini kwamba wajumbe 26 wa Polisario walikuwa katika ndege hiyo.
Mamlaka inajaribu kutafuta mabaki ya waliouawa. Picha kutoka eneo hilo zinaonyesha moshi ukifuka kutoka kwa vifusi vya mabaki ya ndege hiyo.
Naibu waziri wa Ulinzi, pia Mkuu wa majeshi ya Algeria, Jenerali Ahmed Gaid Salaha amezuru eneo la ajali.
Tume ya uchunguzi imeundwa ili kujua sababu ya ajali hiyo.