Pata taarifa kuu
RWANDA-DRC-FDLR

Jeshi la Rwanda katika ardhi ya DRC

Jeshi la Rwanda limevuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amethibitisha Jumanne hii Aprili 19 Mkurugenzi wa mawasiliano wa kanda ya 34 ya jeshi la Congo (FARDC) Kapteni Guillaue Ndjike Kaiko.

Wanajeshi wa DRC (FARDC) katika operesheni Kaskazini mwa mji wa Goma,Oktoba 31, 2013.
Wanajeshi wa DRC (FARDC) katika operesheni Kaskazini mwa mji wa Goma,Oktoba 31, 2013. REUTERS/Kenny Katombe
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Radio Okapi, Kapteni Ndjike Kaiko ameyafahamisha hayo wakati alipokua akiwaonyesha waandishi wa habari matokeo ya uchunguzi wa ujumbe wa jeshi ulioendesha Jumanne hii asubuhi katika vijiji vya Kabagana ya 2 na Chegera, katika eneo la Kibumba, wilayani Nyiragongo (Kivu Kaskazini).

Ujumbe huu ulikua na jukumu la kuchunguza na kukusanya ushahidi kutoka kwa raia na viongozi wao kuhusu tuhuma za kuwepo kwa askari wa Rwanda katika ardhi ya Congo.

Kulingana na ushuhuda wa wakazi wa maeneo hayo, mamia ya askari wa jeshi la Rwanda walivuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Congo wakipitia katika eneo la mpaka lenye namba 123 Jumamosi Aprili 16 mpaka.

Kulingana na wakazi wa maeneo hayo na viongozi wao, askari hawa wa Rwanda wamedhibiti eneo lenye urefu wa kilomita mbili kwenye shule ya msingi ya Upendo na Amani katika kijiji cha Chegera, kwenye umbali wa kilomita thelathini kaskazini mwa mji wa Goma.

Askari hawa wa jeshi la Rwanda wamevuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Congo "kuwasaka waasi wa Kihutu wa Rwanda (FDLR) katika shule ya eneo la Buhumba, " mashahidi wamesema.

Raia hao pia wamesema kwamba askari wa Rwanda wamewaeleza kuwa shule ya msingi ya Upendo na Amani ni moja ya ngome za kundi la waasi wa FDLR. Hata hivyo raia hao wamebaini kwamba hawajawahi kumuona mpiganaji hata mmoja wa FDLR katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika kanda ya 34 ya kijeshi na msemaji wa operesheni Sokola2, Kapteni William Ndjike Kaiko amehakikisha kuwa eneo hilo sasa ni salama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.