Pata taarifa kuu
BURKINA FASO-SHAMBULIO

Burkina: shambulio la kigaidi dhidi ya hoteli Ouagadougou

Shambulio la kigaidi dhidi ya hoteli na mgahawa katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, sehemu zinazotembelewa na watu wengi kutoka nchi za Magharibi, limesababisha vifo vya watu wengi Ijumaa hii usiku.

Picha za hoteli ya Splendid, ikiwaka moto, baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha, Januari 15, 2016.
Picha za hoteli ya Splendid, ikiwaka moto, baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha, Januari 15, 2016. © REUTERS/Reuters TV
Matangazo ya kibiashara

Watu wenye silaha walitawanyika katika hoteli ya Splendid, katika kipindi kisiozidi miezi miwili baada ya shambulio kama hilo lilioendeshwa na wapiganaji wa Kiislamu kutokea nchini Mali.

Milio ya risasi na milipuko ya mabomu vimesikika saa 1:45 usiku (saa za Burkina Faso) katika hoteli ya Splendid na mgahawa wa Cappuccino ulio jirani ya hoteli hiyo. Sehemu hizo zinazotembelewa na watu wengi kutoka nchi za Magharibi zinapatikana katikati mwa mji wa Ouagadougou.

Magari kadhaa yamekua yakiwaka moto kwenye mtaa wa Kwame Nkrumah, moja ya ya maeneo makuu ya katikati mwa mji mkuu ambapo kunapatikana sehemu hizo. Vikosi vya usalama viliwasili katika maeneo hayo baada ya saa moja kutokea shambulio hilo.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Aqmi limekiri kuhusika na shambulio hilo, ambalo linaendelea. Watu kadhaa wameshikiliwa mateka.

Tayari vikosi maalumu vimeanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hili la magaidi ili kujaribu kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa. Taarifa ambayo haijathibitishwa inaeleza kuwa watu zaidi ya ishirini wameuawa katika shambulio hilo.

Itakua kazi ngumu kwa vikosi vya usalama kwani hoteli ya Splendid ina vyumba 147, na watu hao wenye silaha wametawanyika katika vyumba hivyo.

Hakuna tangazo lolote ambalo limekwishatolewa na kiongozi yeyote mpaka sasa, wakati ambapo shambulio hili ni changamoto kwa serikali ya Rais Roch Marc Christian Kaboré, ambaye amechaguliwa hivi karibuni.

Ubalozi wa Ufaransa umebaini kwenye matandao wake kuwa "shambulio hilo ni la kigaidi" na kutoa wito kwa "kuepuka eneo hilo". Eneo hilo limezingirwa na vikosi maalumu pamoja na polisi. Ndege ya shirika la Air France ambayo ilikua njiani ikielekea Ouagadougou, imelazimika kutua kwa dharura katika nchi jirani ya Niger.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.