Pata taarifa kuu
UINGEREZA-BRAZIL-SOKA

Kocha Mkuu wa Uingereza Hodgson afurahishwa na matokeo ya sare dhidi ya Brazili kwenye mchezo uliopigwa Maracana

Kocha Mkuu wa Timu ya taifa ya Uingereza Roy Hodgson amewasifu wachezaji wajke kwa namna ambavyo wamecheza katika kipindi cha pili cha mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Brazil uliopigwa katika Dimba la Maracana. Hodgson amekiri licha ya kucheza vibaya katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo lakini walifanikiwa kuonesha kiwango na uwezo wao katika kipindi cha pili cha mchezo huo na kufanikiwa kupata matokeo ya sare ya magoli 2-2.

Wachezaji wa Uingereza Wayne Rooney na Frank Lampard wakishangilia goli lililofungwa na Alex Oxlade-Chamberlain katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Brazil
Wachezaji wa Uingereza Wayne Rooney na Frank Lampard wakishangilia goli lililofungwa na Alex Oxlade-Chamberlain katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Brazil
Matangazo ya kibiashara

Kocha huyo amesifu sana namna ambavyo safu ya ulinzi ya Uingereza ilivyoweza kuwabana wachezaji wa Brazil ambao walikuwa mwiba katika muda mwingi wa mchezo huo hasa kipindi cha kwanza.

Hodgson hakuwa mchoyo wa fadhila pale ambapo alikiri kuingia kwa Alex Oxlade-Chamberlain kulisaidia pakubwa kubadili mwelekeo wa mchezo huo ambapo alifanikiwa kufunga goli la kusawazisha.

Brazil ilikuwa ya kwanza kupata goli katika mchezo huo uliopigwa kwenye Dimba la Maracana kupitia Mshambuliaji wake Fred goli ambalo lilisawazishwa na Oxlade-Chamberlain aliyefunga goli kwa ufundi mkubwa.

Uingereza ilipata goli la pili kupitia Wayne Rooney ambalo walidhani lingetosha kuwapa ushindi kwenye mchezo huo huko Maracana lakini ndoto zao zilizimwa kwa goli la Paulinho na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare.

Kocha Mkuu wa Brazil maarufu kama Samba Boys Luiz Felipe Scolari amesifu wachezaji wake kwa namna walivyocheza na kusema walicheza na watu wenye uzoefu mkubwa waliotumika timu ya Uingereza Three Lions kwa muda mrefu.

Scolari amesema ni matokeo mazuri kwa vijana wake ambao wanajiandaa kwa mashindano ya Kombe la Mabara yatakayofanyika nchini Brazil baadaye mwezi wa sita na anaamini mchezo huo utakuwa umewasaidia kuona mapungufu yao.

Huu ulikuwa mchezo wa pili baina ya Samba Boys na Three Lions kwani katika mchezo wa kwanza uliopigwa mwezi Februari katika Dimba la Wembley ulishuhudia Uingereza wakiwachakaza Brazil kwa magoli 2-1.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.