rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Uingereza EU Boris Johnson

Imechapishwa • Imehaririwa

Brexit: Boris Johnson aandaa kampeni yake ya uchaguzi

media
Siku ya kwanza ya kampeni ya Boris Johnson haikuwa kama ilivyopangwa Alhamisi hii, Septemba 5, West Yorkshire. Danny Lawson/PA Wire/Pool via REUTERS

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, ambaye ameazimia kufanya uchaguzi wa mapema nchini humo, anasafiri kwenda Scotland leo Ijumaa kuandaa kampeni yake ya uchaguzi.


Hayo yanajiri wakati ambapo Bunge la Seneti linatarajiwa kupitisha sheria kuhusu kuahirishwa kwa mchakato wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit) ifikapo Oktoba 31.

Baada ya kuwatembelea wakulima, Boris Johnson kutoka chama Conservative atapokelewa na Malkia Elizabeth katika kasri yake ya Balmoral.

Wakati huo huo Mahakama Kuu ya Haki jijini London inatarajia kutoa uamuzi wake leo Ijumaa mchana kuhusu rufaa dhidi ya uamuzi wa Boris Johnson wa kusitisha shughuli za Bunge. Kesi hiyo ilianzishwa na mwanaharakati anayepinga Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, Gina Miller, ambaye alishirikiana na na Waziri Mkuu wa zamani kutoka chama cha Conservative John Major.

Hatua hiyo ya kusitisha shughuli za Bunge kwa muda wa wiki tano, hadi Oktoba 14, ambayo imeelezwa kama ujanja wa kuharakisha nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya bila mkataba, imesababisha hasira upande wa upinzani lakini pia na baadhi ya wabunge kutoka chama cha Conservative walipinga hatu hiyo.

Jumatano wiki hii, Baraza la wawakilishi lilipitisha muswada unaomtaka Waziri Mkuu kuomba Brussels kuahirisha mchakato wa kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kwa kipindi cha miezi tatu, hadi tarehe 31 Januari 2020 ikiwa hakuna makubaliano yoyote yatakayo kuwa yamefikiwa na Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 19. Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya - ambao unaweza kuwa nafasi ya mwisho kwa London kumaliza mkataba na umoja huo - umepangwa kufanyika Oktoba 17-18 jijini Brussels, nchini Ubelgiji.

Hayo yanajiri wakati Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amemlaumu kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn kwa kukwamisha muswada wa kutaka nchi hiyo kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu tarehe 15 mwezi Oktoba kutokana na mzozo wa Ungereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Boris sasa anatarajiwa kupendekeza tena muswada huo mapema wiki ijayo kutafuta uungwanji mkono wa wabunge, suala ambalo wachambuzi wanasema huenda hatafanikiwa tena.

Kiongozi huyo anataka Uingereza ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya kufikia tarehe 31 mwezi Oktoba na mkataba au bila ya mkata, suala ambalo wabunge wengi hawataki.

Katika hatua nyingine, Jo Johnson, Waziri wa biashara ambaye pia ni kaka yake mdogo Boris, ametangaza kujiuzulu baada ya kusema kuwa ameshindwa kutofautisha masuala ya familia na kazi, hasa kipindi hiki kigumu cha mzozo wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.