Urusi kuendelea kuwa tayari kutumia silaha za nyukilia: Rais Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwa mara nyengine amesema nchi yake itaendelea kuwa tayari kutumia silaha zake za nyukilia na kwamba Moscow haitovumilia vitisho vyovyote kutoka kwa nchi za Magharibi.
Imechapishwa:
Aidha, amewapongeza wanajeshi wake wanaopigana Ukraine ambapo amezituhumu nchi za Magharibi kwa kuchangia katika mizozo inayoshuhudiwa duniani.
Akizungumza wakati wa gwaride ya kuadhimisha siku ya ushindi wa nchi yake dhidi ya Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia, Putin amewakumbusha raia wa nchi yake kuwa, wanakabiliwa na kipindi kigumu ambacho watashinda.
Rais Putin ameendelea kusisitiza kuwa, vita vya sasa vinayoendelea nchini Ukraine ni vita vya dhidi ya utawala wa kinazi.
Mapema wiki hii, rais Putin aliviagiza vikosi vya nchi yake kwa ushirikiano na wanajeshi wa maji walio kwenye mpaka na nchi ya Ukraine kufanya mazoezi ya silaha za nyukilia.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, vilitangaza kuwa gwaride hilo lingehudhuriwa na viongozi kutoka nchi nane ambazo ni washirika wa karibu wa Urusi.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na wale kutoka katika nchi za Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Turkmenistan, pamoja na Cuba, Laos na Guinea-Bissau, mataifa ambayo Kremlin inasema ni rafiki zake.
Hotuba ya rais Putin imekuja wakati huu wanajeshi wa nchi yake wakiripotiwa kuendelea kupiga hatua katika uwanja wa vita nchini Ukraine.
Putin mwenye umri wa miaka 71, wiki hii ameapishwa tena kuiongoza nchi yake kwa kipindi kingine cha miaka sita baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa mwezi Machi ambao hata hivyo ulisusiwa na upinzani.