Urusi kuzipa nafaka nchi sita za bara Afrika
Nairobi – Rais wa Urusi Vladimir Putin ametangaza mpango wa kuzipa nchi sita maskini za bara Afrika nafaka bila malipo, tangazo la Putin likija siku chache baada ya nchi yake kujiondoa kwenye mkataba wa usafirishaji wa nafaka na Ukraine.
Imechapishwa:
Wiki iliyopita, Moscow ilikataa kuongeza muda wa mkataba huo ambao ulikuwa unatoa nafasi kwa nchi ya Ukraine kusafirisha nafaka yake kupitia kwenye bahari nyeusi kwenda masoko ya kimataifa ikiwemo Afrika.
Wakati akihutubia mkutano wa bara Afrika na Urusi, rais Putin ameahidi kutuma nafaka kwa mataifa sita ya bara Afrika katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Nchi ambazo zitanufaika na mpango huo wa Urusi ni pamoja na Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea.
Putin amesema nchi yake imepanga kuzipa nchi hizo kati ya tani 25,000 hadi tani elfu 50,000 za nafaka.
Mkataba huo ulikuwa unaruhusu usafirishaji wa karibia tani milioni 33 za nafaka kutoka katika bandari za nchini Ukraine na kusaidia katika kukabiliana na uhaba wa chakula.
Viongozi 17 kutoka katika mataifa ya bara Afrika akiwemo rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa siku mbili.
Kremlin imezituhumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kuyazua mataifa ya Afrika kuhudhuria kongamano hilo.